In Summary

•Gari lililohusika katika ajali hiyo linasemekana kuwa la mmoja wa wanasiasa wakuu walioandamana na vinara wa OKA.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenyekiti wa KANU Gideon Moi wakihutubia umma katika kituo cha biashara cha Kyumbi kando ya barabara ya Mombasa kaunti ya Machakos.
Image: GEORGE OWITI

Mwanamume mmoja alifariki huku mwingine akiugua majeraha baada ya pikipiki ambayo walikuwa wameabiri kugongwa na gari lililokuwa kwenye msafara wa One Kenya Alliance  uliozuru kaunti ya  Machakos Jumamosi.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Machakos, Moss Ndiwa alisema kisa hicho kilitokea kando ya barabara ya Kyumbi-Machakos, mita chache tu kutoka mochari ya Montezuma Monalisa.

Gari lililohusika katika ajali hiyo linasemekana kuwa la mmoja wa wanasiasa wakuu walioandamana na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa KANU Gideon Moi kwenye zoezi la uhamasishaji wa usajili wa wapigakura lililofanyika  katika uwanja wa Mulu Mutisya.

Kisa hicho kilitokea wakati msafara wa magari ulipokuwa ukielekea mjini Machakos kwa hafla hiyo.

"Tukio hilo lilitokea kati ya Hoteli ya Lysak na chumba cha kuhifadhia maiti cha Montezuma Monalisa wakati gari kutoka msafara wa wanasiasa lilipomgonga mtu aliyekuwa kwenye pikipiki na abiria wake," Ndiwa alisema.

Mkuu huyo wa polisi alisema mmoja wa wanaume hao alifariki alipokuwa anapokea matibabu katika hospitali ya Machakos Level 5.

Alisema mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ukisubiri kufanyiwa upasuaji huku aliyejeruhiwa akiendelea kupokea matibabu katika kituo hicho.

View Comments