In Summary

• Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ameweka bayana kuhusu madai ya mwanaume kuibiwa pesa alipokuwa akijivinjari katika klabu chake cha Volume VIP huko Shanzu, kwenye kaunti ya Mombasa.

• Akielezea haya katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook, Sonko ametofautiana vikali na Habari zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, na haswa kupitia ukurasa wa DCI.

Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ameweka bayana kuhusu madai ya mwanamume kuibiwa pesa alipokuwa akijivinjari katika klabu chake cha Volume VIP huko Shanzu, kwenye kaunti ya Mombasa.

Akielezea haya katika ukurasa wake wa Facebook, Sonko ametofautiana vikali na Habari zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, na haswa kupitia ukurasa wa DCI.

Sonko amepuuzilia mbali madai ya DCI kwamba mwanamume huyo aliibiwa katika klabu chake na kusema kwamba kitendo cha kuibiwa pesa zake kilifanyika mbali na sehemu hiyo ya burudani baada ya wawili hao kuondoka hapo.

Sonko pia amesema sehemu hiyo ya burudani ina wafanyikazi wenye nidhamu ya juu sana na vile vile iko na kamera za CCTV ambazo zinafanya kazi saa ishirini na nne kwa siku ili kuhakikisha usalama wa wateja wao uko imara.

Mgahawa wa Volume VIP, Shanzu
Image: Facebook

“Ninasema kwamba madai yaliyorekodiwa na DCI ni ya uongo na yanalenga kutuchafulia jina sisi kama Volume VIP Club,” Sonko aliandika.

Vile vile Mike Sonko amesema madai ya kima cha takribani laki sita anazodai kuibiwa mwanamume huyo si ya kweli kwani tayari usimamizi wa sehemu hiyo ya burudani umeshapata taarifa za vile alituma pesa  kwa M-Pesa inayoonyesha kuwa jamaa huyo alituma shilingi elfu 17 pekee kwa akaunti ya huyo mwanadada baada ya maelewano na si kushrutishwa kama  alivyoandika kwa taarifa ya DCI.

“Hata kama sehemu yetu ya burudani ina wajibu wa kuhakikisha usalama wa wateja wetu wote, lakini pia sisi tunahimiza wateja kujiwajibisha katika maamuzi yao binafsi wakiwa ndani ya klabu hichi,” aliandika Sonko.

“Kwa kuwahakikishia wateja wetu wapendwa usalama wao, kuanzia sasa kwenda mbele tunawashauri kuwa makini na kuchukua tahadhari na watu wanaokutana nao katika klabu yetu kwa sababu hili litahakikisha usalama kamili ka kuzuia matukio kama hayo katika siku za baadae,” alishauri Sonko.

View Comments