In Summary

•Konstebo Samuel Ngatia ambaye alikuwa kwenye kikosi cha usalama cha Naibu Rais William Ruto alifariki baada ya kujipiga risasi kichwani Jumatatu asubuhi.

•Ngatia, 35, alikuwa na watoto wawili. Inaonekana alikuwa ametengana na mke wake miaka miwili iliyopita, rafiki wa familia alisema.

Konstebo Samuel Ngatia aliyefariki kwa kujitoa uhai nyumbani kwake.
Image: HISANI

Afisa wa polisi ambaye amekuwa akifanya kazi  katika kitengo cha kusindikiza rais alifariki kwa kujitoa uhai  katika nyumba yake mjini  Juja, Kaunti ya Kiambu.

Konstebo Samuel Ngatia ambaye alikuwa kwenye kikosi cha usalama cha Naibu Rais William Ruto alifariki baada ya kujipiga risasi kichwani Jumatatu asubuhi.

Kilichopelekea tukio hilo bado hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi.

Alikuwa peke yake nyumbani kwake ndani ya kambi ya kikosi cha General Service, kitengo cha  Recce iliyo kando ya Barabara ya Kenyatta wakati wa kisa hicho.

Maafisa waliofika katika eneo la tukio walisema marehemu alitumia bastola yake kufyatua  kichwa chake na  uchunguzi wa awali unaonyesha risasi iliingia upande wa kulia wa kichwa chake na kutokea upande wa kushoto

Bastola aina ya Jericho iliyokuwa na risasi 13 na bunduki aina ya Trevor Sub Machine Gun ikiwa na magazine mbili zilizokuwa na risasi 30 zilipatikana ndani ya nyumba hiyo.

Polisi pia walipata katriji mbili zilizotumika na kichwa kimoja cha risasi.

Mwili wa marehemu ulipelekwa  kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Ngatia, 35, alikuwa na watoto wawili. Inaonekana alikuwa ametengana na mke wake miaka miwili iliyopita, rafiki wa familia alisema.

"Hakuonekana kuwa na msongo wa mawazo tulipokutana Ijumaa iliyopita na tunasubiri taarifa kutoka kwa polisi kuhusu tukio hilo," alisema mwanafamilia wa karibu.

Timu ya wapelelezi kutoka Thika na Juja wanachunguza tukio hilo.

Matukio kama haya yamekuwa yakiongezeka katika idara ya polisi  huku kukiwa na wito wa kushughulikia hali hiyo.

Uhusiano wa maafisa wa polisi na familia zao, wafanyakazi wenzao na wazee miongoni mwa masuala mengine umetambuliwa kuwa baadhi ya sababu za matukio hayo.

Mamlaka za polisi zilipokea ripoti kuhusu sababu za kupigwa risasi na maafisa wa polisi wakiwalenga wenzao.

Uchunguzi huo ulifanywa na timu ya maafisa wakiongozwa na Aggrey Adoli kwa nia ya kubaini sababu na pia hatua za kurekebisha.

View Comments