In Summary

•Wapelelezi wamesema kurudi tena katika eneo la tukio siku ya Alhamisi ni  sehemu ya ukusanyaji wa ushahidi. 

• Uchunguzi wa mwili wa marehemu utafanywa upya Mei 13 na unachukuliwa kuwa ni sehemu ya ukusanyaji wa ushahidi.

Sankok

Timu ya wapelelezi kutoka Kitengo cha kuchunguza Mauaji katika DCI ilichukua jukumu la uchunguzi wa kifo cha mwanawe Mbunge Maalum David Sankok kwa kurudi tena katika eneo ambapo mwili wa marehemu ulipatikana katika Kaunti ya Narok. 

Timu iliunda upya eneo ili kuwawezesha "kujibu maswali mengi ambayo hayajajibiwa", ili kuweza kupata historia ya risasi ya muuaji na kukusanya ushahidi zaidi. 

Walisema kurudi tena katika eneo la tukio siku ya Alhamisi ni  sehemu ya ukusanyaji wa ushahidi.

Haya yanajiri kabla ya kupangwa kwa uchunguzi wa pili wa mwili wa Memusi Sankok, 15, ambaye inasemekana alijipiga risasi na kujiua nyumbani kwa babake katika kaunti ya Narok mnamo Mei 2.

 Uchunguzi wa mwili wa marehemu utafanywa upya Mei 13 na unachukuliwa kuwa ni sehemu ya ukusanyaji wa ushahidi.

Mwanapatholojia mkuu wa Serikali Johansen Oduor ataongoza zoezi hilo mjini Nakuru ambapo mwili huo unahifadhiwa Uchunguzi wa awali wa maiti ulionyesha kuwa kifo cha Memusi kilisababishwa na risasi kwenye kidevu chake na kutoka juu ya kichwa chake. 

Uchunguzi wa kitaalamu uliopangwa utahusisha kuchunguza jeraha la risasi, mwelekeo ambao risasi ilichukua na hata ganda ambalo linaweza kuhusisha matumizi ya X-ray.

 Maafisa walisema uchanganuzi mwingine utakuwa wa mabaki ya risasi ili kuangalia ikiwa kuna uchafu kwenye kiganja cha marehemu ikiwa kweli ndiye aliyefyatua risasi. 

Wakati bunduki inapigwa risasi, uchafu hutoka kwenye bunduki na kubaki kwenye mkono au nguo za yule aliyeshikilia silaha.

GSR pia inaweza kubainisha umbali wa mdomo wa silaha na mlengwa. 

"Je silaha Ilikuwa kwenye kidevu wakati ilifyatuliwa au mbali? Hiyo ni sehemu ya uchunguzi wa kitaalamu unaoendelea,” alisema mkuu wa DCI Mwenda Ethaiba Narok.

 Bunduki mbili zilizopatikana ndani ya nyumba ya Sankok, bastola na bunduki aina ya shotgun, tayari zilikuwa zimesalimishwa kwa ajili ya uchunguzi wa balestiki.

Kijana huyo anasemekana alitumia bunduki hiyo kujiua. Uchanganuzi wa kibalestiki unatafuta kubaini ikiwa bunduki inayohusishwa na tukio hilo ndiyo iliyotumika na ikiwa kweli kichwa cha risasi kilitoka kwa silaha hiyo.

Timu hiyo inachunguza jinsi mtoto huyo alivyoweza kutumia bunduki hiyo kufuatia ugomvi na babake baada ya kudaiwa kukataa kurejea shuleni.

Mbunge huyo aliwaambia wapelelezi kuwa baada ya mabishano yao, alitoka nje ya nyumba na kuelekea hotelini na akiwa huko ndio mwanawe alifika kwenye sefu hiyo, akachukua bunduki na kujipiga risasi.

Baada ya upelelezi kukamilika, wapelelezi wanatarajiwa kupeleka faili kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.

View Comments