In Summary

• Baadhi ya mataifa yanayowakilishwa kwenye kongamano hilo la Kisumu ni mwenyeji Kenya, Somalia, Afghanstan, Marekani na Ufilipino.

• Masuala mengine ambayo yanatarajiwa kushughulikiwa na wajumbe ni uchumi na fedha, kawi, usawa wa kijinsia, ubunifu, uhamiaji na huduma za afya katika sehemu za miji.

• Kongamano hilo la Africities ambalo huandaliwa kila baada ya miaka 3 Barani Afrika linaanza leo tarehe 17 mwezi Mei hadi tarehe 21.

 

Rais Uhuru Kenyatta akiwasili kwa kongamano la Africities Mjini Kisumu, alilakiwa na waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa 17/5/2022.
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amejiunga na wakilishi wa kimataifa Jijini Kisumu kwenye kongamano la kushughulikia changamoto zinazotokana na ukuaji wa miji ulimwenguni.

Kongamano hilo ambalo ni la pili kuwahi kufanyika nchini Kenya baada ya lile la Nairobi miaka tisa iliyopita limewaleta pamoja wakilishi wa serikali mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kijamii, taasisi za masomo na sekta ya kibinafsi.

Baadhi ya mataifa yanayowakilishwa kwenye kongamano hilo la Kisumu ni mwenyeji Kenya, Somalia, Afghanstan, Marekani na Ufilipino miongoni mwa mengine mengi kwa lengo la kuangazia ubora wa makaazi, usimamizi wa miji, utunzi wa sheria na mabadiliko ya hali ya anga.

Masuala mengine ambayo yanatarajiwa kushughulikiwa na wajumbe ni uchumi na fedha, kawi, usawa wa kijinsia, ubunifu, uhamiaji na huduma za afya katika sehemu za miji.

Ni kwa misingi hii ambapo Rais Kenyatta anaongoza ujumbe wa Kenya kuonyesha jamii ya kimataifa zile hatua madhubuti ambazo serikali yake imetekeleza katika kutimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo ikiwemo makaazi bora yaliyo nafuu, uzalishaji, kilimo pamoja na afya bora kwa wote.

Kongamano hilo la Africities ambalo huandaliwa kila baada ya miaka mitatu Barani Afrika linaanza leo tarehe 17 mwezi Mei hadi tarehe 21 Jijini Kisumu kwa hisani ya Serikali ya Kitaifa, Serikali ya Kaunti ya Kisumu pamoja na  Muungano wa Miji Mikuu Barani.

Maudhui ya kongamano la mwaka huu ni "Wajibu wa Miji ya kadri Barani   Afrika katika Utekelezaji wa Ajenda ya mwaka 2030 ya Umoja wa Mataifa na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063".

Miongoni mwa wanaohudhuria kongamano hili ni wakilishi wa nchi na serikali mbalimbali, Waziri Eugine Wamalwa, Gavana wa Kaunti ya Jiji la Kisumu Prof Peter Anyang’ Nyong’o na mwenzake wa Kisii James Ongwae.

View Comments