logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Malala aomba msamaha baada ya kudai mtu anahitaji miguu na mikono tu ili kujiunga na polisi

Malala alisema kazi ya polisi haihitaji elimu yeyote bali inahitaji uwezo wa kushika bunduki tu.

image
na Radio Jambo

Yanayojiri26 May 2022 - 04:07

Muhtasari


•Seneta Malala alisema kazi ya polisi haihitaji elimu yeyote bali inahitaji uwezo wa kushika bunduki tu.

•Malala sasa amesema kuwa ameyaondoa matamshi yake ambayo alisisitiza kuwa yalichukuliwa vibaya.

Seneta wa Kakamega Cleopas Malala ameomba radhi kufuatia matamshi aliyotoa Jumanne ambayo yalilenga idara cha polisi.

Akihutubia wakazi wa Kakamega katika mkutano wa Kenya Kwanza, Malala alisema kazi ya polisi haihitaji elimu yeyote bali inahitaji uwezo wa kushika bunduki tu.

"Bora vijana wana  miguu mbili na mikono mbili waende wafanye kazi katika polisi. Kwa sababu kazi ya polisi nikushika bunduki tuu pekee ake. Hiyo inahitaji masomo kweli?" Malala alisema Jumanne.

Seneta huyo alitaka waliofaulu mitihani waruhusiwe kuendelea na masomo katika vyuo vikuu na waliokatizamasomo waajiriwe katika kitengo cha polisi.

Matamshi hayo yalizua hisia tofauti miongoni mwa Wakenya baadhi wakimkosoa seneta huyo wa muhula wa kwanza huku wengine wakimtetea.

Baada ya kuwa gumzo kubwa mitandaoni Malala hatimaye alijitokeza na kuwaomba polisi msamaha kufuatia matamshi yake. 

Kupitia taarifa aliyotoa Jumatano jioni, Malala alisema kuwa ameyaondoa matamshi yake ambayo alisisitiza kuwa yalichukuliwa vibaya.

"Ningependa kusema kwa kina kwamba matamshi yangu yalichukuliwa nje ya muktadha kabisa. Umuhimu wao (polisi) kwetu hauwezi kupuuzwa. Ni kutokana na hili kwamba ningependa kufuta matamshi yangu na kuomba radhi kwa vikosi vyetu vilivyo na nidhamu kwa usumbufu ambao matamshi yangu yanaweza kusababisha," Malala alisema kupitia Facebook.

Katika ujumbe wake wa msamaha, Malala ambaye anawani ugavana wa Kakamega katika uchaguzi wa Agosti 9 aliwataja polisi kama "Wanaume na wanawake wetu wenye nidhamu katika sare."

Haya yalijiri muda mfupi tu baada ya idara ya polisi kupitia msemaji wao Bruno Shioso kukashifu matamshi ya seneta huyo na kusema yanasikitisha.

Shioso alisema matamshi ya Malala yanadhalilisha sana na yanalenga kukashifu taaluma ambayo imetukuka.

"Tumesikitishwa zaidi kwa kuwa matamshi haya ya kusikitisha yalitolewa na kiongozi ambaye sio tu kwamba tunamheshimu sana lakini pia tunaendelea kumpatia ulinzi wa siku nzima  kwa fahari na umahiri," Shioso alisema.

Msemaji huyo wa polisi aliweka wazi kuwa maarifa ni hitaji kubwa katika huduma ya polisi na bunduki ni chombo cha ziada tu cha kuwezesha kazi zao.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved