In Summary

• NMS ilikuwa imetangaza mapema kwamba majaribio ambayo yalipangwa kufanyika kwa awamu yataendelea hadi Jumapili, Juni 26, wakati mawasiliano zaidi yatakapofanywa. 

• Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Matatu, Simon Kimutai alikosoa vile jaribio hilo liliendeshwa na kupelekea kufeli kwake. 

Image: WILFRED NYANGERESI

Huku ikiwa chini ya saa sita baada ya jaribio la kutumia kituo cha Matatu cha Green Park jijini Nairobi kuanza, Nairobi Metropolitan Services iliamuru matatu kurejea katikati mwa jiji. 

Hii ilikuwa baada ya wahudumu wa matatu na wasafiri kukemea kwa sana, mirundiko ya watu na foleni ndefu za magari hali iliyotatiza jaribio hilo lililokuwa limeanza Jumatano asubuhi. 

NMS ilikuwa imetangaza mapema kwamba majaribio ambayo yalipangwa kufanyika kwa awamu yataendelea hadi Jumapili, Juni 26, wakati mawasiliano zaidi yatakapofanywa. 

Jaribio la Jumatano zilikusudiwa tu kwa matatu zinazotumia njia za Rongai, Kiserian, Ngong, Karen, Lang'ata, Nairobi West/Madaraka, Kibra, Kawangware, Dagoretti/Satellite, Kilimani, Highrise/Ngumo na Kikuyu.

 Hata hivyo, kabla ya saa sita mchana, matatu zilikuwa zimerejea kwenye vituo vyao vya kawaida katikati mwa jiji (CBD) Railways, Agro house na Kencom miongoni mwa vituo vingine. 

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Matatu, Simon Kimutai alikosoa vile jaribio hilo liliendeshwa na kupelekea kufeli kwake. 

"Wasanifu wa miji walifanya kazi duni na ni dhahiri kuwa Nairobi haina wapangaji wazuri wa mifumo ya uchukuzi," alisema. 

Kimutai pia alisema kituo hicho kiliwekwa upande usiofaa wa jiji jambo ambalo litasababisha msongamano mkubwa zaidi. 

Kimutai alikosoa zaidi NMS kwa kukosa kushauriana na wamiliki wa matatu na badala yake kushauriana na watu wasio wadau katika sekta ya uchukuzi wa umma.

 "Ushauri ni muhimu na bila hivyo, jiji hili halitajinasua kwenye barabara zenye misongamano," alisema. 

Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa majaribio hayo yatasalia kufeli kutokana na kutokuwepo kwa maeneo ya kugesha magari yanayosubiri kuingia jijini kuchukuwa abiria.

 "Hawajatoa viwanja bado wanataka matatu tatu kwa kila Sacco ndani ya kituo? Huu ni mzaha," Kimutai aliongeza. 

Matatus zikiwa zimerejea katika steji ya mabasi ya Railways baada ya majaribio ya Nairobi Metropolitan Services ya kituo cha Greenpark kufeli mnamo Juni 22, 2022.
Image: WILFRED NYANGERESI

Kulingana na wahudumu wa matatu, majaribio hayo yalikuwa na changamoto zinazowaathiri moja kwa moja na kutatiza shughuli za kila siku ambazo wamezoea.

"Tunachukua muda mwingi kuingia kwenye kituo ikilinganishwa na hali yetu ya kawaida ambapo tunashuka tu na kuchukua sehemu moja," John Akama, dereva alilalamika. 

Changamoto nyingine ni ukosefu wa abiria hasa nyakati za asubuhi. Wahudumu wa matatu walilalamika kuwa pindi waliposhukisha abiria  ndani ya kituo walilazimika kuondoka bila abiria kwani hapakuwepo na abiria wa kubeba.

 "Tofauti na hatua zetu za awali, hakuna biashara hapa bado haturuhusiwi kupiga kambi kubeba abiria. Tunaondoka bila wasafiri,” alisema Julius Wafula. 

Licha ya changamoto katika kituo cha Green Park, wahudumu wa matatu walisema nauli imesalia ile ile. 

Abiria wengi walitaabika sana kwa kutembea mwendo mrefu kuingia ndani ya jiji huku wengine waliokuwa na watoto wadogo wakihangaika hata zaidi.

View Comments