In Summary
  • Rais alionyesha kushtushwa na kifo cha ghafla cha kiongozi huyo wa zamani wa Japan na kumtaja kama rafiki na mshirika wa maendeleo wa taifa la Kenya
Aliyekuwa waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta ameungana na viongozi wa dunia kuomboleza aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe aliyefariki siku ya Ijumaa baada ya kupigwa risasi kwenye mkutano wa kampeni za kisiasa.

Rais alionyesha kushtushwa na kifo cha ghafla cha kiongozi huyo wa zamani wa Japan na kumtaja kama rafiki na mshirika wa maendeleo wa taifa la Kenya.

Katika ujumbe wake wa rambi rambi ulisoma;

"Inashangaza sana na kwa kiasi fulani haiaminiki kujua kuhusu kifo cha rafiki yangu, na mmoja wa washirika wakuu wa maendeleo wa Kenya, Waziri Mkuu wa zamani Shinzo Abe, katika tukio la kupigwa risasi kikatili," Uhuru alisema.

Waziri Mkuu wa zamani Abe, ambaye alistaafu mwaka wa 2020, alitembelea Nairobi mwaka wa 2016 wakati wa mkutano wa 6 wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD), ambapo alifanya mazungumzo na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

Shinzo alifariki baada ya kupigwa risasi alipokuwa akitoa hotuba ya kampeni ya uchaguzi katika jiji la Nara, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

Mtangazaji wa NHK na shirika la habari la Kyodo liliripoti kifo cha Abe siku ya Ijumaa, saa chache baada ya mzee huyo wa miaka 67 kupigwa risasi kifuani na shingoni.

Hata hivyo polisi walimkabili mshukiwa wa shambulizi dhidi ya Abe.

 

 

 

View Comments