In Summary

•Mashahidi na polisi walisema moto huo ulizuka kwenye kantini ya taasisi hiyo dakika chache kabla ya saa kumi na mbili asubuhi ya Jumatatu. 

•Polisi walisema walikuwa wamearifiwa kuwa kikosi cha zima moto hakikuweza kujibu kwa sababu lori zao hazina bima. 

Moto ulizuka katika kantini ya KBC mnamo Julai 11, 2022. Maafisa walilalamika kuwa hakuna jibu kutoka kwa kikosi cha zima moto cha kaunti-
Image: HISANI

Moto uliteketeza sehemu ya kantini katika taasisi ya utangazaji ya serikali- Kenya Broadcasting Corporation (KBC) na kusababisha hofu katika eneo hilo. 

Mashahidi na polisi walisema moto huo ulizuka kwenye kantini ya taasisi hiyo dakika chache kabla ya saa kumi na mbili asubuhi Jumatatu. 

Chanzo cha moto katika jengo hilo ambalo liko kando ya Barabara ya Harry Thuku hakikubainika mara moja. 

Hii ilizua hofu huku wafanyikazi wa KBC wakihamishwa na wengine waking’ang’ana kuzuia kuenea. 

Polisi walisema hakuna majeruhi ambao waliripotiwa katika tukio hilo lakini mali ya thamani isiyobainishwa iliharibiwa. 

Chumba kiliathiriwa kipo karibu na studio za utangazaji. 

Polisi, maafisa wa G4S na mashirika mengine ya kibinafsi hata hivyo waliudhibiti moto huo wakitumia lori la kukabiliana na moto baada ya kucheleweshwa kwa mara ya kwanza na serikali ya kaunti ya Nairobi, ambayo inasemekana haikuwa na gari la zima moto. 

Huduma za utangazaji ziliendelea kawaida zaidi ya saa moja baadaye. 

Polisi walisema walikuwa wamearifiwa kuwa kikosi cha zima moto hakikuweza kujibu kwa sababu lori zao hazina bima. 

Maafisa katika kituo cha kupokea simu walisema katika kipindi cha wiki moja ambacho kimepita wamekuwa katika hali ya kuchanganyikiwa kwa kukosa majibu kutoka kwa kikosi cha zima moto cha Kaunti kinachodai kuwa lori hizo hazina bima.  

“Wanasema lori zao hazina bima na hivyo hawawezi kujibu matukio hayo. Tuna changamoto kubwa hapa,” Alisema afisa mmoja ambaye aliomba jina lake lisitajwe. 

Afisa huyo alisema kisa kama hicho cha moto kilichotokea Jumapili katika mtaa wa Kangemi kiliharibu majengo mengi kwa sababu kikosi hicho hakikujibu. 

Kisa kama hicho kilitokea katika mitaa ya mabanda ya Mukuru, polisi walisema na kuongeza kuwa wanahofia mkasa mkubwa bila majibu kutoka kwa watoa huduma muhimu. 

"Tunalazimika kutafuta usaidizi kutoka kwa kikosi cha zima moto cha kibinafsi na wakati mwingine wanajeshi, jambo ambalo ni gumu na linalotia wasiwasi," aliongeza afisa huyo. 

Kikosi cha zima moto kwa sasa kinasimamiwa na Nairobi Metropolitan Services na serikali ya kaunti. 

Gavana Anne Kananu alisema watashughulikia suala hilo. Aliahidi kulishughulikia haraka iwezekanavyo. 

Maafisa wanahofia maafa makubwa yanaweza kutokea kwa sababu ya ukosefu wa mwitikio kutoka kwa kikosi cha zima moto na wanataka itolewe kipaumbele.

View Comments