In Summary

•Marehemu alisema hakutaka kuendelea kusababisha matatizo zaidi shuleni humo na katika harakati hizo kumfanya mama yake kuteseka kwa sababu yake.

•Msichana huyo alibainisha kuwa alikusudia kukatisha maisha yake na kwenda kukutana na baba yake.

Marehemu Francisca Dokee
Image: HISANI

Barua ya kujitoa uhai inayodaiwa kuachwa na msichana wa kidato cha tatu katika shule ya upili ya Tala Girls,  Kaunti ya Machakos ambaye alifariki kwa kujitoa uhai imeibuka.

Katika barua hiyo, marehemu Francisca Dokee alilaumu uongozi wa shule hiyo kwa kutoamini maelezo yake kwamba hakuhusika kamwe  na wizi wa mali za wanafunzi wenzake kama ilivyodaiwa. 

"Ninaelezea kitu, mnaunda yenu wenyewe. Niliwaambia kuwa sihusiki na penseli zilizopotea, lakini bado mnaamini katika hisia zenu kwamba mimi ndiye," Barua hiyo iliyofikia  Radio Jambo ilisoma.

Msichana huyo ambaye alikuwa na umri wa miaka 16 alipokumbana na kifo chake mnamo Agosti 31 aliendelea kueleza kuwa uamuzi wa kukatisha maisha yake ni kwa sababu hakutaka kuendelea kusababisha matatizo zaidi shuleni humo na katika harakati hizo kumfanya mama yake kuteseka kwa sababu yake.

Pia alichukua fursa hiyo kueleza upendo wake kwa mamake na kakake mdogo ambaye pia alitakia heri katika mtihani wa KCPE.

"Kwa mama yangu, kwaheri na ninakupenda sana. Unachukua nusu ya moyo wangu huku kaka akichukua nusu nyingine. Natumai Mungu abariki kazi ya mikono yako na pia niombee kakangu afaulu katika KCPE yake,"

MAREHEMU Fransisca Dokee akiwa na mama yake Magdalene Mueni katika picha ya maktaba.
Image: HISANI

"Ninaomba na kutumai kwamba hamtamhusisha mama yangu katika hili kwa sababu anaweza kufa haraka sana na bado ana kazi kadhaa za kufanya kwa ndugu zangu. Natumai," Marehemu aliwaambia walengwa.

Msichana huyo alibainisha kuwa alikusudia kukatisha maisha yake na kwenda kukutana na baba yake.

"Kwaheri, nakuja kukutana nawe baba," Aliandika.

Mwanafamilia mmoja wa marehemu ambaye aliandamana na mamake Magdalene Mueni, wakati wa uchunguzi wa maiti katika Hospitali ya Kangundo Level 4 siku ya Ijumaa pia alisoma barua hiyo kwa wanahabari.

Barua inayodaiwa kuachwa na marehemu Francisca Dokee
Image: HISANI

Alikuwa ameambatana na Mueni pamoja na jamaa wengine aliposoma barua hiyo.

Uchunguzi wa maiti  ulifichua kwamba msichana huyo alikufa kwa kushindwa kupumua, uthibitisho kwamba alijitoa uhai..

"Uchunguzi wa maiti imefichua kuwa mtoto alifariki kwa kujitoa uhai. Ni sawa," Mwanafamilia huyo alisema.

Hata hivyo, alilaumu usimamizi wa shule kwa kifo cha msichana huyo wao.

Kulingana na polisi, kifo cha msichana huyo kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Tala mnamo Agosti 31 chini ya OB NO: 37/8/2022 1540HRS kama ripoti ya tukio la kujitoa uhai..

View Comments