In Summary

• Brig. Lekolool alikuwa miongoni mwa ADCs watatu ambao walimhudumia Rais Uhuru Kenyatta  kwa miaka 10 kabla ya kustaaafu.

Kanali Fabian Lengusuranga akiwa Nyeri ambapo Rais William Ruto anahudhuria mazishi ya kakake Naibu Rais Rigathi Gachagua Oktoba 4, Picha: PSCU

Kanali Fabian Lengusuranga kutoka Jeshi la nchi kavu ndiye mlinzi au ADC mpya wa Rais William Ruto. 

Anachukua usukani kutoka kwa Brigedia Timothy Stelu Lekolool kutoka Jeshi la Wanamaji la Kenya ambaye ametumwa katika Makao Makuu ya Idara ya Ulinzi. 

Lengusuranga siku ya Jumanne aliandamana na Ruto hadi Nyeri, ambako anahudhuria mazishi ya kakake naibu wa Rais Rigathi Gachagua aliyefariki wiki jana. 

Mlinzi huyo mpya atasaidiwa na Luteni Kanali Damaris Agnetta pia kutoka Jeshi la nchi kavu. Anachukua nafasi ya Racheal Nduta Kamui ambaye amepandishwa cheo hadi Kanali kamili na kutumwa katika makao makuu ya Idara ya Ulinzi. 

Kanali Lengusuranga alifuzu mwaka wa 1999.

Yeye ni afisa wa kijeshi aliye na uzoefu na amekuwa akihudumu kama kamanda mkuu wa Kikosi Maalum. Agnetta alifuzu mwaka 2003 na amekuwa afisa wa Udhibiti wa Mizinga.

Pia amehudumu katika Ujumbe wa Waangalizi wa Umoja wa Mataifa. Kulingana na Baraza la Ulinzi, mabadiliko hayo hufanyika mara kwa mara kwa sababu ya maendeleo ya kazi ya maafisa. Uteuzi wa ADC kawaida hufanywa baada ya kushauriana na Baraza la Ulinzi la Kitaifa. 

Muda ambao ADC huhudumu hutegemea masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na umri, lakini wengi wao wanahudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu. 

Brig. Lekolool alikuwa miongoni mwa ADCs watatu ambao walimhudumia Rais Uhuru Kenyatta  kwa miaka 10 kabla ya kustaaafu.

Alikuwa ADC wa kwanza kuchaguliwa kutoka Jeshi la Wanamaji. Lekolool alikuwa ADC wa Uhuru hadi Septemba 13, William Ruto alipoapishwa.

View Comments