In Summary

•Mwili huo uligunduliwa siku ya Jumanne na kuwashangaza wakaazi waliokuwa wakitumia maji hayo nyumbani.

•Kwingineko, polisi walisema miili miwili iligunduliwa Jumanne kando ya barabara katika eneo la Kikuyu.

crime scene

Maafisa wa upelelezi wameanzisha uchunguzi baada ya miili mitatu kupatikana katika maeneo tofauti mjini Kiambu.

Moja ya miili hiyo iligunduliwa kwenye kisima cha maji katika mtaa wa Mifereli, Kiambaa.

Polisi na wanakijiji walisema mwanamume mmoja alikuwa akisafisha kisima chenye urefu wa futi 110 ambacho kimekuwa kikitumika lakini maji yake yamekuwa yakipungua wakati aligundua mwili uliokuwa ukioza humo ndani.

Kulingana na polisi, mwanamume huyo alitambuliwa baadaye kuwa Bernard Njuguna, 30, ambaye alitoweka miezi miwili iliyopita.

Mwili huo uligunduliwa siku ya Jumanne na kuwashangaza wakaazi waliokuwa wakitumia maji hayo nyumbani.

Mamake Njuguna aliwaambia polisi kwamba mwanawe alitowela Oktoba na amekumbwa na mfadhaiko mkubwa tangu wakati huo.

Haijulikani ikiwa alikufa kwa kujitoa uhai au alitupwa humo au alianguka kwa bahati mbaya.

Mwili ulihamishwa hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Kwingineko, polisi walisema miili miwili iligunduliwa Jumanne kando ya barabara katika eneo la Kikuyu.

Wanakijiji walisema waligundua miili miwili ya wanaume wazima wasiojulikana ikiwa imelal kando ya Barabara ya Kikuyu-Dagoretti.

Polisi waliitwa kwenye eneo la tukio na kusema kuwa mwili mmoja ulikuwa umefungwa kipande cha kitambaa shingoni na kwamba miili yote miwili ilikuwa na majeraha yanayoonekana.

Mabaki ya mchanga yaliyopatikana kwenye miguu yao yalionyesha kuwa waliuawa mahali pengine na miili hiyo kutupwa hapo.

Polisi walihamisha miili hiyo hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City ikisubiri uchunguzi .

Mkuu wa polisi wa Kiambu Perminus Kioi alisema bado hawajatambua miili hiyo miwili na juhudi za kufanya hivyo zinaendelea.

Sababu bado haijajulikana lakini polisi walitaja matukio hayo kuwa mauaji, ambayo yanachunguzwa.

Ugunduzi huo ni wa kawaida katika eneo hilo huku miili mingi ikitupwa humo.

Polisi wanasema waathiriwa wanauawa kwingine kabla ya kutupwa katika maeneo tofauti eneo hilo.

Kesi nyingi zinaendelea chini ya uchunguzi, polisi walisema.

(Utafsiri: Samuel Maina)

View Comments