In Summary

• Waziri aliagiza idara ya wizara husika kuunda kamati ya kuongoza uundaji wa mfumo wa utekelezwaji wa hazina hiyo ndani ya siku 30.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI KITHURE KINDIKI
Image: KWA HISANI

Serikali mwezi ujao itazindua hazina maalum ya ufadhili kwa familia na wanaotegemea maafisa wa polisi na magereza ambao wanafariki wakiwa kazini.

Waziri wa Mambo ya Ndani Prof. Kithure Kindiki alitangaza hayo siku ya Ijumaa wakati wa ibada ya kuwakumbuka maafisa 53 katika Chuo cha Mafunzo cha Polisi cha Kenya Embakasi.

Alisema fedha hizo zitatolewa ndani ya siku 30 kwa ajili ya kusaidia familia zilizofiwa kukabiliana na hali ngumu ya maisha kufuatia kuondokewa na wapendwa wao.

"Hazina hiyo itachangisha fedha kusaidia familia ambazo zimeachwa nyuma katika kupata ufadhili wa chini kwa watoto na matibabu kwa wale ambao wameachwa kama tegemezi, na aina zingine za dharura za elimu, afya," Kindiki alisema.

Waziri aliagiza idara ya wizara husika kuunda kamati ya kuongoza uundaji wa mfumo wa utekelezwaji wa hazina hiyo ndani ya siku 30.

"Ripoti hiyo itajumuisha jinsi hazina hiyo itakavyofanya kazi, usimamizi, ili tusaidie kukusanya rasilimali kutoka kwa serikali na mahali pengine kutoka kwa washirika wetu," alibainisha.

Kindiki alifichua kuwepo kwa mpango wa serikali kuajiri angalau mtu mmoja kutoka familia ya afisa aliyefariki katika vikosi hivyo viwili akisema kuwa tayari wajane sita na mayatima watatu katika mpango wa majaribio wanatarajiwa kufuzu mwaka huu.

Kuhusiana na uboreshaji wa vifaa, Kindiki alisema kuwa zana za kinga na usafiri wa nchi kavu, anga na baharini vitatiliwa maanani ili kukinga maafisa dhidi ya hatari ya mashambulizi.

View Comments