In Summary

•DP alifanya ziara ya  Mlima Kenya kwa mara ya pili katika siku mbili mfululizo asubuhi ya leo, Jumamosi, Januari 7.

•Naibu rais pia aliwaombea vijana waweze kukombolewa kutoka kwa matumizi ya dawa za kulevya na mambo mengine maovu.

Naibu Rais Rigathi Gachagua alifanya ziara ya Mlima Kenya ambapo aliombea nchi ya Kenya.
Image: TWITTER// RIGATHI GACHAGUA

Naibu Rais Rigathi Gachagua alifanya ziara ya  Mlima Kenya kwa mara ya pili katika siku mbili mfululizo asubuhi ya leo, Jumamosi, Januari 7.

Katika taarifa aliyochapisha kwenye Twitter, Gachagua ambaye ni miongoni mwa viongozi waliokusanyika Mt Kenya Safari Club mjini Naivasha  kwa kongamano la siku chache alisema alitembea kupanda mlima na akafurahia mazingira.

"Nilipokuwa nikipitia Mawingu Trail, niliona wanyamapori mbalimbali wanaotuzunguka. Swala wa majini na swala wa kawaida," naibu rais alisema.

Kiongozi huyo wa pili kwa utawala alibainisha kwamba alifurahia mandhari na hali ya hewa ya msitu wa Mlima Kenya wakati wa ziara yake.

Pia alidokeza kwamba alifanya sala tena huko mlimani ambapo alimuombea rais William Ruto pamoja na Wakenya wote kwa jumla.

"Niliomba kwamba Mungu atupe mvua ili watu wetu wanaofanya kazi kwa bidii waweze kuona tena na kufurahia matunda ya kazi yao kutoka katika mashamba yao," alisema.

Naibu rais pia aliwaombea vijana waweze kukombolewa kutoka kwa matumizi ya dawa za kulevya na mambo mengine maovu.

"Naamini kwamba Mungu amesikia maombi yangu. Mlima ni shwari. Mlima iko sawa. Kenya iko kwenye njia sahihi," alisema Gachagua.

Siku ya Ijumaa asubuhi, naibu rais alifichua kwamba alifanya ziara isiyo ya kawaida ya Mlima Kenya ambapo alichukua muda kutafakari.

"Niliamka mapema leo saa kumi asubuhi ili kufanya safari ya hisia kuelekea Mlimani. Safari ya saa moja ambayo ilijumuisha kuvuka Mto Rikkia ilinikumbusha juu ya mapambano makubwa ya uhuru wetu," alisema kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Gachagua pia alifichua kwamba alichukua muda kufanya sala na kumshukuru Maulana kwa wema wake kwa Wakenya.

Pia alimuombea rais William Ruto na aweze kuwa na afya afya njema na maarifa ya kuongoza taifa la Kenya.

"Nikiangalia Mlima Kenya, nilimuomba 'Mwene Nyaga' ampe afya njema na hekima Kiongozi wetu Mkuu Rais @WilliamsRuto anapoanza mageuzi ya kiuchumi ya taifa letu na kurejesha utu wa watu wa Kenya," alisema.

Naibu rais pia aliwahakikishia Wakenya kwamba eneo la Mlima Kenya bado liko sawa na thabiti.

View Comments