In Summary

•Ajali hiyo ambayo ilitokea siku ya Jumamosi usiku mwendo wa saa nne katika eneo la Kakwamunyen pia ilisababisha watu wengine 12 kujeruhiwa.

•Walionusurika walisema kuwa dereva wa gari hilo mwenye umri wa miaka 32 alilalamikia maumivu ya kifua kabla ya ajali hiyo.

Lori na eneo ambapo watu 14 waliuawa na 12 kujeruhiwa Jumamosi Februari 4 katika ajali kwenye Barabara kuu ya Lodwar-Kakuma.
Image: HISANI

Takriban watu 14 wamefariki katika ajali iliyotokea kwenye barabara kuu ya Lodwar-Kakuma, kaunti ya Turkana.

Ajali hiyo ambayo ilitokea siku ya Jumamosi usiku mwendo wa saa nne katika eneo la Kakwamunyen pia ilisababisha watu wengine 12 kujeruhiwa.

Ripoti ya polisi iliyofikia Radio Jambo inaonyesha kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya dereva kushindwa kulidhibiti gari hilo akikwepa kumgonga ngamia.

Waliouawa ni pamoja na wanawake wazima wanane, wanaume wazima watatu na vijana watatu wa kiume

"Ilitokea kwamba gari lilikuwa likiendeshwa kuelekea upande wa Kakuma na baada ya kufika eneo la ajali kulikuwa na ngamia aliyekuwa akivuka barabara kutoka kushoto kwenda kulia."

“Dereva aligeukia upande wa kulia ili kukwepa kuligonga na kutokana na uzito wa gari hilo kutokana na mizigo iliyokuwemo na abiria, ndipo aliposhindwa kulidhibiti gari hilo, likapinduka na kutua kwenye mtaro,” taarifa ya polisi inasoma kwa sehemu.

Manusura wote walikimbizwa katika Kaunti ya Lodwar na kupelekwa hospitali kwa matibabu huku maiti zikihamishwa hadi katika chumba kimoja cha kuhifadhia maiti zikisubiri kufanyiwa uchunguzi.

Walionusurika walisema kuwa dereva wa gari hilo mwenye umri wa miaka 32 alilalamikia maumivu ya kifua kabla ya ajali hiyo.

Dereva pia alikuwa amebeba bidhaa mbalimbali za duka wakati wa ajali.

Peter Lomorukai, Afisa Mkuu wa Kinga na Afya katika Serikali ya Kaunti ya Turkana, alisema wamepokea waathiriwa waliohusika katika ajali mbaya katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Lodwar na wanaendelea na matibabu.

Alisema hali ya wagonjwa hao ni nzuri na hali ni shwari.

Polisi walisema wanachunguza tukio hilo.

View Comments