In Summary

• Madzayo alisema kuwa spika alikwenda kinyume na maadili ya Bunge na mfano uliowekwa na watangulizi wake.

FATUMA DULLO

Muungano wa Azimio umepata pigo katika jitihada za kumtimua seneta wa Isiolo Fatuma Dullo kama kiranja wa wachache katika Seneti baada ya mahakama kusitisha kwa muda hatua hiyo. 

Naibu Spika wa Seneti Kathure Murungi alisema kuwa spika Amason Kingi amepokea agizo kutoka kwa Mahakama ya Mizozo ya Vyama vya Kisiasa kumzuia kufanya mabadiliko hayo.

 "Kwa hivyo ninaahirisha uwasilishaji wa mawasiliano hadi suala hilo litakaposikilizwa na kuamuliwa," Murungi alisema. 

Spika alitarajiwa kufanya mawasiliano ya kumuondoa Dullo Jumanne mchana. Katika mabadiliko hayo, Dullo anatazamiwa kubadilishwa na seneta wa Narok Ledama Ole Kina ambaye amekuwa Naibu wake. 

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna anatarajiwa kuwa Naibu wa Ole Kina. Lakini kiongozi wa wachache Stewart Madzayo amepinga hatua hiyo akisema yeye na chama chake bado hawajapokea maagizo hayo ya mahakama. 

Madzayo alisema kuwa spika alikwenda kinyume na maadili ya Bunge na mfano uliowekwa na watangulizi wake. Alisema kuwa PPDT haina mamlaka ya kusimamisha shughuli za Bunge. 

"Tunachotaka sisi wachache, ni tulichowapa wiki iliyopita na kimechukua muda mrefu, sasa mnawanyima fursa upande wa wachache kuwa na viongozi wao," alisema.

View Comments