In Summary

•Mwathi alipatikana amefariki baada ya kudaiwa kuanguka kutoka kwa ghorofa ya 10 ya jumba ambalo DJ Fatxo anaishi.

•DCI ilisema kitengo cha kuchunguza mauaji  kilichukua kesi hiyo kufuatia agizo la mkuu wa DCI, Bw Mohamed Amin.

Ibada ya mazishi ya Jeff Mwathi
Image: HISANI

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imeahidi uchunguzi wa kina katika kesi ya kifo cha kijana wa miaka 23, Geoffrey Mwathi, aliyepatikana amefariki katika mazingira ya kutatanisha takriban wiki mbili zilizopita.

Mwathi, almaarufu Jeff, alifariki mnamo Februari 22 na ripoti iliyoandikishwa katika kituo cha polisi iliashiria kwamba alijitoa uhai kwa kuruka  kupitia dirisha la nyumba ya mwimbaji maarufu wa Mugithi, DJ Fatxo.

Taarifa iliyotolewa na DCI siku ya Ijumaa ilisema kitengo cha kuchunguza mauaji cha idara hiyo kilichukua kesi ya kifo cha kijana huyo ambaye ni binamu ya Samidoh kufuatia agizo la mkuu wa DCI, Bw Mohamed Amin.

"Umma umehakikishiwa kuwa hakuna jiwe ambalo halitapinduliwa katika upelelezi wa kesi hii na mtu yeyote atakayebainika kuhusika na kifo hicho atakabiliwa na mkono wa sheria," taarifa ya DCI ilisoma.

Kufuatia hilo, wapelelezi walitoa wito kwa umma kutoa taarifa yoyote ambayo itasaidia katika uchunguzi.

Hapo awali, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kindiki Kithure aliagiza mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, Mohamed Amin kufanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo..

“Kuhusu suala la marehemu Jeff Mwathi, tumezungumza na DCI Amin na kumwagiza atume kikosi cha wauaji kutoka makao makuu ya DCI kuchunguza kwa kina kisa hicho na kuchukua hatua zinazohitajika,” Kindiki alisema.

Waziri alithamini juhudi za wapelelezi hao katika kushughulikia suala hilo.

"Timu ya kuchunguza mauaji kutoka makao makuu ya DCI haina upendeleo, na hii itasaidia kutatua madai ya kula njama," alisema.

Mwathi alipatikana amefariki baada ya kudaiwa kuanguka kutoka kwa ghorofa ya 10 ya jumba ambalo DJ Fatxo anaishi.

Mwimbaji huyo na wenzake waliandikisha taarifa katika kituo cha polisi ambapo walidai kwamba Mwathi alijitoa uhai kwa kuruka chini kupitia dirisha ya nyumba yake usiku wa kuamkia tarehe 22 Februari.

Walisema kijana huyo alikuwa na mawazo ya kujitoa uhai kabla ya hatimaye kuyatekeleza siku hiyo.

Familia ya Mwathi hata hivyo imetupilia mbali madai kwamba alikuwa na mawazo ya kujitoa uhai huku sasa wakidai majibu.

View Comments