In Summary

•Murkomen amemteua Kapteni William Ruto kama mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA).

•Nafasi ya Mkurugenzi katika KPA imekuwa wazi kwa miaka 3 iliyopita.

Kapteni William Ruto ambaye ni MD mpya wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya
Image: KPA

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amemteua Kapteni William Ruto kama mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA).

Kapteni Ruto atahudumu katika wadhifa wake mpya kwa miaka mitatu ijayo.

"Waziri wa Barabara na Uchukuzi amemteua Kapteni William K Ruto kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya, kwa muda wa miaka mitatu (3), kuanzia Machi 10, 2023," notisi ya gazeti la serikali ilisema.

Nafasi ya Mkurugenzi katika KPA imekuwa wazi kwa miaka 3 iliyopita.

Kapteni Ruto ni baharia mzoefu aliyeanza kazi yake mwaka wa 1991 katika KPA kama Afisa wa sitaha ya baharini kabla ya kupanda vyeo na kuwa Meneja Mkuu wa Uendeshaji kazi na baadaye Mwalimu wa Bandari.

Kabla ya uteuzi huu, alikuwa Meneja Mkuu wa Bandari ya Kisumu.

"Ni imani yangu kwamba uzoefu wake wa miaka 32 utasaidia sana katika kuhakikisha Mamlaka inatekeleza wajibu wake kwa watu wa Kenya na inaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa Kenya," CS Murkomen alisema.

"Ninampongeza Mkurugenzi Mkuu mpya na kumhakikishia uungwaji mkono wa Serikali katika usimamizi wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya."

Kapteni William Ruto ana shahada ya Uzamili katika Utawala wa Biashara (MBA) Usimamizi wa Mikakati kutoka Chuo Kikuu cha JKUAT.

Yeye pia ni mshirika wa Taasisi ya Nautical (AF-NI) na mwanachama wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ualimu wa Bandari (Uingereza), na amepata sifa ya juu zaidi kama Nahodha wa Meli (Class 1 Master Mariner) kutoka Chuo cha Bahari cha Tyneside Kusini, Uingereza.

View Comments