In Summary

•Mwili huo uligunduliwa mapema Jumatatu, siku chache baada ya kichwa cha mwanaume kugunduliwa mahali hapo hapo.

•Mkono mwingine ulionekana umekuliwa na mbwa mwitu.

Wakaazi wa Raganga, Kitutu Chache Kusini, Kisii wakusanyika katika eneo la tukio ambapo mwili usio na kichwa uligunduliwa mnamo Aprili 10, 2023.
Image: MAGATI OBEBO

Wakazi wa kijiji cha Raganga, katika eneo la Kitutu Chache Kusini, kaunti ya Kisii walipigwa na butwaa baada ya kupata mwili usio na kichwa uliotupwa kwenye kichaka.

Mwili huo uligunduliwa mapema Jumatatu, siku chache baada ya kichwa cha mwanaume kugunduliwa mahali hapo hapo. Ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Wakaazi wanashuku kuwa huenda kichwa kilichopatikana awali kilitenganishwa na mwili wa marehemu uliopatikana Jumatatu asubuhi.

Mwili huo haukuwa na miguu na mkono mmoja, jambo lililoibua tuhuma za uwezekano wa mauaji.

Mkono mwingine ulionekana umekuliwa na mbwa mwitu.

Kathogo Ayienda, mkazi wa kijiji hicho alisema bado hawajamtambua marehemu.

Alisema huenda aliuawa kwingine na mwili wake kutupwa katika eneo lao.

"Hivi majuzi ilikuwa kichwa, leo kiwiliwili kimeletwa hapa. Tunataka kujua nani anahusika na mauaji haya na kwa nini wanatupa miili hapa," Ayienda alisema.

Sasa wanataka polisi wachunguze.

"Polisi wachunguze watuambie, inaweza kuwa mauaji ya kikatili? Atoke mtu atoe maelezo," Ayienda alisema.

Tayari mwili huo umepelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Mkuu wa Polisi wa Kitutu Chache Kusini Anthony Keter alisema uchunguzi unaendelea.

"Tuko kwenye suala hilo na tutatoa muhtasari wa kina mara tutakapomaliza," alisema.

View Comments