In Summary

Viongozi wa Bungoma wamedai kuwa usalama umezidi kuwa hafifu wakilalamikia uzembe wa polisi kazini.

watu watatu wakamatwa kwa madai ya kuhusika na kifo cha mhubiri eneo la Mlima Elgon.
Image: HISANI

Washukiwa watatu wanaoshutumiwa kuhusika na kifo cha mhubiri wa eneo la Mt Elgon wamekamatwa.

Kulingana na DCI, washukiwa hao wamewekwa kwenye rumande kwa kuhusika na kifo cha David Ngeiwa ambaye aliuawa kinyama  tarehe 7, Machi 2023 katika eneo la Kaptama, Mt Elgon kaunti ya Bungoma.

"Washukiwa watatu wako kwenye rumande sasa kufuatia kifo cha Mhubiri David Sylvester Ngeiwa aliyeuawa kinyama," DCI walisema.

Visa vingi vya utovu wa usalama vimeripotiwa katika eneo hilo la Mlima Elgon huku viongozi wa eneo hilo wakimtaka Inspekta Jenerali wa polisi, Japhet Koome kuchukua hatua mwafaka ili kudhibiti usalama wa wananchi wa eneo hilo dhidi ya makundi ya majambazi.

"Maafisa hawa itabidi wahamishwe, sitakaa tu nikitazamwatu wangu wakiwa hatarini," ,alisema seneta wa Bungoma Wafula Wakoli.

"Tunataka haki kwa mhubiri huyu. Tunataka kujua ni jambo lipi wauwaji wake walikuwa nalo juu yake ndipo wakamuua. Tumekuwa tukifurahia usalama hapa, hatutaki kurudi kwa siku za awali za giza," alisema naibu gavana wa Bungoma , Jeniffer Mbatiany.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa pia alisema kuwa uhamisho wa maafisa wa eneo hilo unafaa kufanywa kwa kuwa wamekua kwa kituo moja cha polisi kwa muda wa miaka 15.

Eneo la Mt Elgon hapo awali limekuwa likikabiliana na magenge ya majambazi ambao walikuwa ni tisho la usalama kwa wakazi wa eneo hilo yakiwemo makundi maarufu ya SLDF na Matakwei. Mzozo wa ardhi ndio umekuwa jambo kuu katika sehemu hizo.

View Comments