In Summary

•Miili saba hadi sasa imetolewa, mbili katika kaburi moja lisilo na kina.

•Eneo hilo lilitambuliwa siku ya Alhamisi na lilikuwa na makaburi 8 lakini mengine 58 yalipatikana katika eneo moja.

Maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha mauaji na wataalam wa uchunguzi waanza kuopoa miili ya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kasisi wa Malindi Paul Mackenzie katika eneo bunge la Shakahola Magarini kaunti ya Kilifi.
Image: ALPHONSE GARI

Maafisa wa kitengo cha mauaji wameanza kufukua miili katika makaburi yanayoaminika kuwa ya wafuasi wa mchungaji Mackenzie.

Miili saba hadi sasa imetolewa, mbili katika kaburi moja lisilo na kina.

Timu ya maafisa wapatao 100 wakiongozwa na Mkurugenzi wa kitengo cha Mauaji pamoja na mwanapatholojia, maafisa kutoka DCI, Idara ya uchunguzi, na polisi wa kawaida wanaongoza operesheni hiyo.

Zaidi ya makaburi 32 yalipatikana. Miili imefunikwa na leso kwenye makaburi.

Zoezi hilo lilianza siku ya Ijumaa majira ya mchana huku Mkurugenzi wa Idara ya mauaji akitoa maelekezo juu ya mchakato huo.

Wananchi hawakuruhusiwa katika eneo la tukio na waandishi wa habari pia walipewa maelekezo ya jinsi ya kujiendesha katika eneo la tukio.

Baada ya takribani masaa mawili ya kuchimba, kulikuwa na dalili kwamba kulikuwa na miili na kwa uangalifu mkubwa mwili mmoja wa mtu mzima ulipatikana ukifuatiwa na miili miwili iliyokuwa imezikwa kwenye kaburi moja.

Eneo hilo lilitambuliwa siku ya Alhamisi na lilikuwa na makaburi 8 lakini mengine 58 yalipatikana katika eneo moja.

Wakati wa kuchapishwa kwa taarifa, kitengo cha mauaji na wataalam wa upelelezi wa mahakamani walikuwa wanafukua makaburi mengine.

Maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha mauaji na wataalam wa uchunguzi waanza kuopoa miili ya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kasisi wa Malindi Paul Mackenzie katika eneo bunge la Shakahola Magarini kaunti ya Kilifi.
Image: ALPHONSE GARI

Wanaharakati wa haki za binadamu kutoka Haki Africa na Malindi Social Justice Centre pia walishuhudia mchakato wa ufukuaji.

Mathias Shipeta wa Haki Africa alisema wamefurahishwa na hatua iliyofikiwa hadi sasa na vyombo vya usalama.

Victor Kaudo alisema Serikali inapaswa kuongeza maafisa ili waweze kuharakisha zoezi la uchimbaji wa maiti ili haki ianze kufuatwa.

Wakati wa operesheni hiyo, waandishi wa habari walikutana na mwanamume mmoja wa Nigeria ambaye alikuwa akiwatafuta wanafamilia wake sita waliotoweka wiki mbili zilizopita.

Alisema mkewe, mtoto na dada zake walifika Malindi na anashuku walifika kwa mchungaji katika eneo la Shakahola.

Katika mahojiano, Mnigeria huyo alisema mkewe aliondoka nyumbani kwake Aprili 8 kuelekea Likoni na kisha akaungana na dada zake kusafiri hadi Malindi.

"Mara ya mwisho nilipompigia simu alikuwa ameenda dukani na alikuwa sawa lakini hajawahi kuwasiliana tena," alisema.

Alisema alisafiri hadi Malindi na kwenda hadi Shakahola kwa kutumia Google Maps hadi alipowakuta polisi wanaoendesha operesheni hiyo lakini hawajawaona wanafamilia yake sita.

Wenyeji waliohojiwa waliishukuru serikali kwa kuendesha shughuli ya kufukua miili ya wafuasi wa Mackenzie.

Hata hivyo waliionya serikali dhidi ya kumwachilia pasta huyo.

View Comments