In Summary

• Wiki iliyopita, Kenya Kwanza ilisema iko tayari kumwondoa mbunge wa Eldas Aden Keynan kwenye mazungumzo hayo.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo
Image: MAKTABA

Waakilishi wa muungano wa Azimio katika mazungumzo ya pande mbili wamesema hawana uwezo kusitisha maandamano yalioitishwa na viongozi wa muungano huo.

Wakihutubia wanahabari Jumanne, waakilishi hao wakiongozwa na Mbunge Otiende Amollo walieleza kuwa kamwe hawakuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

"Kama kamati ya pamoja ya vyama viwili, hatukuwahi kupewa mamlaka ya kujadili chochote kuhusu maandamano. Sio katika nafasi yetu kuitisha au kusitisha maandamano," Otiende alisema.

Otiende alibainisha kuwa baadhi ya masuala yaliyoibuliwa na muungano wa Kenya Kwanza hayakuwa na msingi.

“Huwezi kumchukua mwanachama wetu ukamweka kwenye kamati kisha urudi na kutuambia tuondoe wetu ili na wewe ufanye hivyo hivyo haina mantiki,” alisema.

Wiki iliyopita, Kenya Kwanza ilisema iko tayari kumwondoa mbunge wa Eldas Aden Keynan kwenye mazungumzo hayo.

Katika kile kinachoonekana kama jaribio la kushawishi upinzani kusitisha maandamano yaliyopangwa, Kenya Kwanza ilisema Keynan ataondolewa ikiwa kutakuwa na mzozo wakati wa majadiliano.

Hata hivyo, Kenya Kwanza pia ilitaka wenzao wa Azimio pia kumwondoa Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing kutoka kwa kamati hiyo.

Aidha, Otiende alisema timu ya Kenya Kwanza haijaondoa jina la Keynan kwenye orodha hiyo, na kuwataka Wakenya wasidanganywe.

View Comments