In Summary
  • Wabunge wanatazamiwa kujadili mswada huo siku ya Alhamisi, huku kukiwa na onyo lililotolewa na Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua
Mwanaharakati Boniface Mwangi
Image: Hisani

Polisi  wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji katika mji mkuu wa Nairobi wanaopinga baadhi ya hatua zinazopendekezwa na serikali za kutoza ushuru mpya au wa juu zaidi kwa bidhaa zikiwemo mafuta.

Mojawapo ya hatua kuu zinazopingwa katika muswada wa fedha ambao unapingwa na wengi ni tozo mpya ya 3% ya nyumba kwa wafanyakazi wote wanaolipwa mishahara na kuongeza ushuru wa ongezeko la thamani kwenye mafuta hadi 16%.

Muswada huo pia unataka kodi kwa bidhaa za urembo, sarafu za mtandani na mapato yatokanao na mitandao ya kijamii. Ni miongoni mwa hatua ambazo zimepingwa na Wakenya wengi.

Makumi ya waandamanaji walikuwa wakijaribu kukusanyika katika bustani moja katikati mwa jiji la Nairobi kabla ya kuandamana hadi bungeni kuwataka wabunge kukataa mapendekezo hayo.

Wabunge wanatazamiwa kujadili mswada huo siku ya Alhamisi, huku kukiwa na onyo lililotolewa na Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua dhidi ya wanaopinga mapendekezo hayo.

Huku mwanaharakati wa haki za binadamu Boniface Mwangi akizungumzia suala hilo alisema kuwa utawala wa Ruto unakuwa utawala wa kidikteta usiovumilia maoni tofauti baada ya kuzuia maandamano ya amani katika Wilaya ya Biashara ya Kati (CBD).

"Kutuma polisi kuwakamata waandamanaji wa amani kwa kutumia haki yao ya kusikilizwa ni tabia ya kidikteta," Mwangi alisema huku akitoa wito kwa serikali kukumbatia maoni tofauti.

Msafara huo kutoka bustani ya Jevanjee jijini Nairobi ulionekana kuwa wa amani hadi kundi la maafisa waliovalia kiraia walipohamia kuwakamata wanaharakati waliokuwa wakiongoza maandamano hayo.

Wanaharakati walikuwa na nia ya kuwasilisha ombi lao kwa Wabunge, lakini juhudi zao zilikwama baada ya maafisa wa kupambana na ghasia kuwavamia na mabomu ya machozi ili kutatiza msafara wao.

 

 

 

 

 

View Comments