In Summary

•Kingeno alijisalimisha katika kituo cha polisi Makimeny, eneo la Chepalungu baada ya kutekeleza mauaji hayo nyumbani kwao kwa kutumia upanga.

•Mshukiwa pia anaripotiwa kujaribu kumuua baba yake ambaye alikimbia katika eneo la tukio baada ya kusikia kelele.

Crime scene

Polisi katika kaunti ya Bomet, mkoa wa Bonde la Ufa wanamzuilia mwanaume mmoja anayedaiwa kumuua mpenziwe wa miaka 25 kwa kutaniana na wanaume wengine kwenye mtandao wa Facebook.

Ismael Kingeno Langat mwenye umri wa miaka 21 anaripotiwa kujisalimisha katika kituo cha polisi Makimeny, eneo la Chepalungu baada ya kutekeleza mauaji hayo nyumbani kwao kwa kutumia upanga.

Kingeno anaripotiwa kumkatakata mpenzi huyo ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu hadi kifo baada ya kuchunguza akaunti yake ya Facebook na kugundua alikuwa akishiriki mazungumzo ya kimapenzi na marafiki wa kiume.

Mshukiwa pia anaripotiwa kujaribu kumuua baba yake ambaye alikimbia katika eneo la tukio baada ya kusikia kelele. Mzazi huyo wake alinusurika kifo baada ya kuondokea upanga ambao mwanawe alitaka kumuua nao.

Baada ya kumuua mpenzi wake, kijana huyo alifululiza moja kwa moja hadi kituo cha polisi huku akiwa amebeba silaha ya mauaji na kujiripoti.

Kingeno alieleza kwamba tayari alikuwa amemuonya marehemu kuhusu tabia ya kutaniana na wanaume ila hakusikia. Aidha, alidai kwamba alilazimika kuuza kipande chake cha ardhi ili kumsomesha mpenziwe katika chuo kikuu. 

Polisi wanaendelea kumzuilia mshukiwa huku mwili wa mpenzi wake ukiwa umehifadhiwa katika makafani ya hospitali ya Longisa.

View Comments