In Summary

•Viongozi wa Azimio wameapa kuendeleza maandamano hadi pale serikali itashughulikia swala la kupanda kwa gharama ya maisha.

IG Koome awaambia Azimo vitisho vya ICC haviwezi kumtisha
Image: STAR

Maandamano yaliopangwa na muungano wa Azimio la umoja siku ya Jumatano ni haramu, hii ni kulingana na Inspekta Mkuu wa polisi Japhet Koome.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne jioni, Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome alisema viongozi wa muungano wa Azimio hawajawasilisha taarifa yoyote rasmi kwa polisi kuhusu maandamano hayo na kwa hivyo ni haramu.

Koome alisema kwamba polisi watatumia njia zote halali kukabili waandamanaji siku ya Jumatano.

“Kwa maslahi ya usalama wa taifa, idara ya Polisi nchini inapenda kuufahamisha umma kuwa wapangaji wa maandamano hawajawapa polisi taarifa kama  sharti la kisheria kuwezesha polisi kutoa ulinzi wa kutosha kwa waandamanaji na wananchi, polisi hawana njia nyingine ila kuchukua hatua zinazohitajika kutawanya maandamano yote haramu,” alisema Koome.

Inspekta mkuu wa polisi alisema kuwa hawataruhusu mtu yeyote kuendeleza maandamano. Maandamano ya Azimio yanajiri huku jiji la Nairobi likiwa mwenyeji wa Rais wa Iran Ebrahim Raisi ambaye aliwasili nchini siku ya Jumatano kwa ziara rasmi ya siku moja.

Viongozi wa Azimio wakiongozwa na kinara wao Raila Odinga wameapa kuendeleza maandamano hadi pale serikali itashughulikia swala la kupanda kwa gharama ya maisha miongoni mwa maswala mengine.

Akizungumza siku ya Jumanne Kinara wa Azimio Raila Odinga aliwataka Wakenya bila kujali mirengo yao ya kisiasa kujitokeza kwa wingi Jumatano kujiunga na maandamano.

Huku hayo yakijiri, Rais William Ruto siku ya Jumanne alitoa onyo kali kwa upinzani, akiapa kutoruhusu maandamano yoyote yenye vurugu na ambayo yanahatarisha maisha ya Wakenya.

Ruto alisema kwamba vifo sita viliripotiwa kutokana na maandamano ya Saba Saba wiki jana, akiongeza kwamba hataunga mkono kifo cha Mkenya yeyote kutokana na maandamano.

Maandamano ya Ijumaa iliyopita ya Saba Saba yalifanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwa ni pamoja na Nairobi, Kisumu, Migori, Homa Bay, Mombasa, Kisii, Kakamega, Kirinyaga, Machakos, Meru na Nyahururu.

View Comments