In Summary

• Azimio ilisema maandamano yataendelea siku ya Alhamisi, na kutangaza "Wakenya wasikate tamaa."

• Rekodi za polisi zinaonyesha kuwa vifo hivyo viliripotiwa katika maeneo ya Nairobi, Wote, Nakuru na Kisumu huku kukiwa na hofu kuwa huenda idadi ya vifo itaongezeka.

• Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na; Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga, kakake Peter Kamunya miongoni mwa wengine.

Mwanamke aliyepigwa risasi wakati wa maandamano ya saba saba huko Kisii afariki
Image: Magati Obebo

Watu wasiopungua sita waliuawa kwa kupigwa risasi na wengine 30 kujeruhiwa katika maeneo tofauti kwenye maandamano ya kuipinga serikali ya Rais William Ruto siku ya Jumatano.

Rekodi za polisi zinaonyesha kuwa vifo hivyo viliripotiwa katika maeneo ya Nairobi, Wote, Nakuru na Kisumu huku kukiwa na hofu kuwa huenda idadi ya vifo itaongezeka.

Zaidi ya watu 30 wanauguza majeraha baada ya makabiliano na polisi. Wengi wa waathiriwa walipigwa risasi katika mitaa ya mabanda ya Nairobi, Nakuru, Kisumu na Makueni. Polisi walisema walikamata zaidi ya watu 300 kwa kushiriki maandamano hayo.

Jijini Nairobi, mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi eneo la Embakasi na mwingine Mathare.

Wengine wawili walipigwa risasi mjini Kisumu, wawili Nakuru na mmoja Emali.

Polisi walisema waathiriwa waliuawa au kujeruhiwa katika makabiliano na polisi wakati wa maandamano siku ya Jumatano. Waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali mbali mbali. 

Maafisa katika Mamlaka Huru ya shughuli za Polisi (IPOA) ambao wameshutumiwa kwa kutofanya juhudi za kutosha katika kutatua matukio ya polisi kutumia vibaya silaha siku za nyuma waliahidi kuchunguza visa hivyo vipya.

Watoto waliojipata katikati ya makabiliano hayo pia wanauguza majeraha katika hospitali mbali mbali.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alisema watu 300 walikamatwa Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru na miji mingine ambapo polisi walikabiliana na waandamanaji.

"Zaidi ya watu 300 wamekamatwa nchini kote na watafunguliwa mashtaka mbalimbali ya uhalifu, ikiwa ni pamoja na uporaji, uharibifu wa mali, kuasha moto, wizi wa mabavu, kuwashambulia polisi na uhalifu mwingine," alisema katika taarifa yake.

Hakuwataja waathiriwa wa risasi katika taarifa yake.

Azimio ilisema maandamano yataendelea siku ya Alhamisi, na kutangaza "Wakenya wasikate tamaa."

"Tutaendelea na maandamano yetu ya amani kama tulivyopanga. Lakini tutasimama saa kumi na moja jioni leo (Jumatano) na kurejea kesho (Alhamisi) asubuhi,” muungano huo ulisema.

Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na; Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga, kakake Peter Kamunya miongoni mwa wengine.

Njenga alikamatwa kutoka kwa nyumba ya babake huko Kiserian na zaidi ya maafisa 50 waliovamia boma la babake Jumatano usiku na kupelekwa mahali pasipojulikana. 

Baada ya kukamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, Babu Owino alipelekwa hadi kituo cha polisi cha Wanguru huko Kirinyaga na kuzuiliwa humo.

View Comments