In Summary

•Bi Ongili alibainisha kuwa mumewe hajafanya lolote baya na akaomba serikali imruhusu amjulie hali na kumpa chakula.

•Bi Ongili alieleza wasiwasi wake kwamba huenda mwanasiasa huyo akahamishwa kutoka Wang’uru hadi eneo lingine.

Bi Fridah Ongili na mumewe Babu Owino
Image: HISANI

Mke wa Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Fridah Ongili ameiomba serikali kumruhusu kuonana na mumewe ambaye anadai anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Wang’uru katika eneo la Mwea, Kaunti ya Kirinyaga.

Kwenye taarifa ya video iliyosambazwa na timu ya Azimio, Bi Ongili alibainisha kuwa mumewe hajafanya lolote baya na akaomba serikali imruhusu amjulie hali na kumpa chakula.

“Hakuna kitu kibaya alichokifanya na nilichokuwa nataka kama mke ni kumpa mume wangu chakula ili ale na kumwangalia tu kuona yuko salama. Ninaomba tu Wakenya au watu wowote wenye nia sawa, yeyote anayeweza kunisaidia anisaidie kumfikia mume wangu,” Bi Ongili alisema.

Alifichua kuwa aligundua kuwa mumewe anazuiliwa Mwea baada ya kumtafuta katika maeneo mengine mengi ikiwa ni pamoja na vituo vya polisi vya Embakasi, Kilimani, Muthaiga, Kileleshwa, uwanja wa ndege na katika makao makuu ya DCI kando ya barabara ya Kiambu.

Hii ilikuwa baada ya mbunge huyo wa ODM kudaiwa kumpigia simu mwendo wa saa tano usiku wa Jumanne kumjulisha kuhusu kukamatwa kwake katika uwanja wa ndege wa JKIA.

"Nilihangaika sana kumtafuta. Hatimaye nilipewa taarifa kwamba yuko katika Kituo cha Polisi cha Wang’uru huko Mwea na tukaja hapa,” alisema.

Alidai kuwa alipofika Wang’uru alikutana na afisa wa kike ambaye alimnyima nafasi ya kumpa mumewe chakula na dawa kwa kuwa alikuwa anaugua.

“Walinikataza kuingia. Hakika walinibeba hadi nje. Langoni kulikuwa na polisi wengi, niliweza kubaini kuwa mume wangu alikuwa katika kituo cha polisi cha Wangu’ru huko Mwea,” alisema.

Bi Ongili alieleza wasiwasi wake kwamba huenda mwanasiasa huyo akahamishwa kutoka Wang’uru hadi eneo lingine lisilojulikana baada ya wao kufanikiwa kujua alikozuiliwa.

Sasa amewataka viongozi wa Azimio wakiongozwa na Raila Odinga kumsaidia mumewe ambaye anasisitiza hana hatia na alikuwa akitetea haki za Wakenya pekee.

View Comments