In Summary

•Etale alidai kuwa mlinzi huyo wa waziri mkuu huyo wa zamani aliachwa katikati ya barabara ya Ruai na gari lake kuharibiwa.

•Kuachiliwa kwa Ogeta kulijiri baada ya mahakama kuamuru awasilishwe mbele ya mahakama yoyote nchini mnamo siku ya Ijumaa.

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga akiwa na mlinzi wake Maurice Ogeta katika Ikulu wakati wa mkutano uliopita.
Image: MAKTABA

Mlinzi wa kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga, Maurice Ogeta sasa ni mtu huru.

Mkurugenzi wa mawasiliano katika chama cha ODM Philip Etale alithibitisha katika taarifa kwamba Ogeta aliachiliwa kutoka mikononi mwa polisi mwendo wa saa saba usiku wa kuamkia Jumamosi.

Etale alidai kuwa mlinzi huyo wa waziri mkuu huyo wa zamani aliachwa katikati ya barabara ya Ruai na gari lake kuharibiwa.

“Maurice Ogeta, mlinzi wa Raila Odinga aliachiliwa kutoka kwa polisi dakika chache kabla ya saa saba usiku na kuendeshwa huku akiwa amezibwa macho na kuachwa katikati ya barabara ya Ruai kuelekea Kangundo. Gari lake limeharibiwa,” Etale alisema siku ya Jumamosi asubuhi.

Aliongeza, "Walakini, anafurahi kuwa hai lakini bado amefadhaika na mshtuko."

Ogeta alikamatwa siku ya Jumatano kwa madai ya kuhusika katika maandamano ya kuipinga serikali. Alikamatwa jijini Nairobi alipokuwa akiendesha gari kuelekea kazini asubuhi ya siku hiyo ya maandamano.

Katika taarifa, Etale alidai kuwa Ogeta alitekwa nyara na kubebwa siku ya Jumatano asubuhi na watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa polisi ambao hawakuwa wamevalia sare.

Alisema Ogeta alitekwa nyara na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa DCI kabla ya kupelekwa kusikojulikana.

"Watu wasiojulikana waliokuwa wamevalia nguo za kawaida wanaoshukiwa kuwa maafisa wa polisi kutoka DCI wamemteka nyara mlinzi wa Raila Odinga Maurice Ogeta alipokuwa akiendesha gari kuelekea kazini, wakamfunga kwenye buti ya gari, na kumpeleka kusikojulikana. Mahali alipo bado hajulikani aliko," Etale alisema Jumatano.

Afisa kutoka huduma ya polisi alithibitisha kuwa Ogeta alikuwa miongoni mwa wale waliolengwa kukamatwa na kuzuiliwa. Alikuwa amefuatwa nyumbani kwake Langata, afisa huyo alisema.

Kulingana na polisi, Ogeta alikuwa akizuiliwa katika seli za kituo cha polisi cha Utawala.

Kuachiliwa kwa Ogeta kulijiri baada ya mahakama kuamuru awasilishwe mbele ya mahakama yoyote nchini mnamo siku ya Ijumaa.

Jaji Lawrence Mugambi alitoa uamuzi huo Ijumaa wakati kesi hiyo ilipowasilishwa mbele yake.

Katika amri yake, jaji Mugambi aliagiza majibu kuhusu suala hilo yawasilishwe na kutolewa ndani ya siku tatu baada ya amri hiyo.

View Comments