logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Waziri Kindiki atoa hakikisho la kukabiliana na Al-shabaab

Serikali sasa itawapa maafisa wa polisi vifaa vya kisasa kukabiliana na waalifu

image
na Davis Ojiambo

Habari18 September 2023 - 14:11

Muhtasari


  • • "Tumetangaza vita dhidi ya al-Shabaab. Wanaweza kufikiri watatuzidi ujanja lakini tutawaangamiza kama vile tulivyofanya wezi wa mifugo."
  • • Aidha alikariri kuwa  serikali haitakubali mauaji ya kiholela, akisema "Siku za kutoweka kwa nguvu zimepita zamani."
Waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki

Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki amesema kuwa serikali haitalegea katika vita dhidi ya kundi al-Shabaab.

Akizungumza katika Kaunti ya Wajir wakati wa operesheni ya Kaunti Ndogo ya Kotulo huko Tarbaj, Kindiki alitaja kundi la wanamgambo kuwa adui mkubwa wa Kenya.

“Huyo ndiye adui yetu mkubwa kwa sasa. Wamesababisha maafa nchini mwao na wanaleta hiyo Kenya. Tumedhamiria kuwa serikali inayorejesha amani katika eneo la Kaskazini Mashariki,” 

Waziri aliendelea kutema moto kwa ghadhabu akisema;

"Tumetangaza vita dhidi ya al-Shabaab. Wanaweza kufikiri watatuzidi ujanja lakini tutawaangamiza kama vile tulivyofanya wezi wa mifugo."

Waziri Kindiki aliwashauri wananchi wote kufanya kazi na maafisa wa usalama na kupinga majaribio ya makundi ya kigaidi ya kuwafanya vijana kuwa na itikadi kali.

Aliongeza kusema kuwa serikali itawapa maafisa wa usalama vifaa vya kisasa ili kuwalinda dhidi ya wahalifu waliojihami na kuwawezesha kuwalinda Wakenya na mali zao.

Hata hivyo, aliwapongeza maafisa wa usalama kutoka kwa mashirika yote kwa kufanya kazi bila kuchoka na kwa bidii ili kupambana na ukosefu wa usalama katika Mkoa wa Kaskazini Mashariki.

“Baadhi ya maafisa wetu hata wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa na wahalifu waliojihami. Hakuna zawadi ya kutosha kuwaheshimu maafisa wetu kwa bidii yao. Ni wanaume na wanawake wazalendo wanaoipenda nchi yao. Natoa pongezi kwa maafisa hawa wote wanaofanya kazi katika eneo gumu la Kaskazini Mashariki,” 

Aidha alikariri kuwa  serikali haitakubali mauaji ya kiholela, akisema "Siku za kutoweka kwa nguvu zimepita zamani."

Waziri Kindiki alisimamia kuanzishwa kwa makao makuu ya Kaunti Ndogo ya Kotulo na kuteuliwa kwa Naibu Kamishna wa kwanza wa Kaunti Farah Hassan Mohamed.

 


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved