In Summary

• Mama wa mtoto huyo alisema mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani asubuhi na mapema, na hakueleza tatizo lolote alilokuwa nalo.

• Mwili wa marehemu ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Rapcom ukisubiri uchunguzi wa maiti na polisi.

Kitanzi
Image: HISANI

Polisi kwa ushirikiano na wasimamizi wa kaunti wameanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha mwanafunzi wa umri wa miaka 12, ambaye anashukiwa kujiua ndani ya darasa la shule ya msingi ya Sare huko Awendo, Kaunti ya Migori.

Chifu wa eneo hilo, Paul Ogweno, alisema mwili wa mwanafunzi wa darasa la nne ulipatikana ukining'inia ndani ya darasa Jumanne asubuhi na wanafunzi waliokuwa wameripoti shuleni.

Ogweno alisema bado hawajabaini kilichojiri kabla ya mvulana huyo kuchukua maisha yake.

Mama wa mtoto huyo alisema mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani asubuhi na mapema, na hakueleza tatizo lolote alilokuwa nalo,

Mwili wa marehemu ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Rapcom ukisubiri uchunguzi wa maiti na polisi.

Wakati huo huo chifu wa eneo hilo ametoa wito kwa wazazi kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na watoto wao ili waweze kujua baadhi ya changamoto wanazopitia.

Alisema watoto wengi wanaweza kuwa na matatizo ya kiakili kwa sababu ya masuala ya kifamilia miongoni mwa mengine. Bila umakini na usaidizi wa kihisia wa wazazi wao huamua kujiua.

Ogweno alisema ipo haja kwa watoto na watu wazima kupata usaidizi muhimu wa kisaikolojia pale wanapokuwa na msongo wa mawazo.

Kaunti ya Migori imekuwa na visa vinavyoongezeka vya magonjwa ya akili kulingana na data kutoka kwa idara ya afya ya kaunti hiyo.

View Comments