In Summary

•Bobi Wine alikuwa ameenda kwa ziara za uhamasishaji nchini Afrika Kusini na Kanada na alitarajiwa kurudi Uganda leo, Oktoba 5.

•Chama hicho kilimshutumu Rais Yoweri Museveni kwa hatua hiyo kikieleza kuwa kukamatwa kwake kulifanywa kwa vurugu.

Bobi Wine
Image: MAKTABA

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu almaarufu Bobi Wine anadaiwa kukamatwa wakati akirejea nyumbani kutoka safarini.

Bobi Wine alikuwa ameenda kwa ziara za uhamasishaji nchini Afrika Kusini na Kanada na alitarajiwa kurudi Uganda leo, Oktoba 5. Kwa mujibu wa chama chake National Unity Platform (NUP), mwanasiasa huyo hata hivyo alikamatwa na maafisa katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe alipotua nchini.

Chama hicho kilimshutumu Rais Yoweri Museveni kwa hatua hiyo kikieleza kuwa kukamatwa kwake kulifanywa kwa vurugu.

"Rais @HEBobiwine amekamatwa," chama cha NUP kilisema kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X.

Chama hicho kiliambatanisha taarifa hiyo na video za madai ya kukamatwa kwa mgombea urais huyo katika uchaguzi wa 2021 katika uwanja wa ndege wa Entebbe.

"Hivi ndivyo rais @HEBobiwine amekamatwa kwa vurugu aliporejea Uganda. Bado hatujajua aliko,” chama hicho kilisema.

Chama hicho pia kilidai kuwa maafisa zaidi walikuwa wametumwa nyumbani kwa Bobi Wine huko Magere, Uganda na kuambatanisha video kuthibitisha madai hayo.

Video zilizoshirikiwa na NUP zilionyesha Bobi Wine akikamatwa vibaya na maafisa wasio na sare mara baada ya kuteremka kutoka kwa ndege. Kisha aliongozwa hadi kwenye gari lililojaa katika uwanja wa ndege kabla ya kupelekwa kusikojulikana.

View Comments