In Summary

• Kamati hiyo itaendelea kujadili ajenda yake yenye vipengele vitano; Mambo ya Kikatiba ambayo hayajakamilika; Haki ya uchaguzi na mambo husika.

Wanachama wa Kenya Kwanza na viongozi wa Azimio la Umoja katika ukumbi wa Bomas of Kenya mnamo Agosti 9. Picha: TEDDY MULEI

Mazungumzo ya pande mbili kati ya chama tawala cha Kenya Kwanza na upande wa Azimio La Umoja yanaendelea leo Jumatano.

Kulingana na taarifa kutoka kwa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo yenye wajumbe 10 inayoongoza mazungumzo hayo yatafanyika faraghani kujadili masuala tata huku yakizingatia pia maoni ya wakenya.

Kamati hiyo itaendelea kujadili ajenda yake yenye vipengele vitano; Mambo ya Kikatiba ambayo hayajakamilika; Haki ya uchaguzi na mambo husika; uanzishwaji wa ofisi za Serikali; na Uaminifu kwa Vyama vya Siasa/Miungano na sheria ya demokrasia ya vyama vingi.

Awali Azimio ilisema itachukua hatua mbadala ikiwa mazungumzo hayo yataonyesha kutokuwa na matumaini.

Odinga na kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka mwezi uliopita walisema upinzani hautapoteza muda katika mazungumzo bila ishara kwamba masuala yao yatashughulikiwa.

"Kabla ya kuzungumzia uchaguzi wa 2027, lazima tusuluhishe 2022 na ndio maana tuna mazungumzo ya pande mbili. Tunataka kusuluhisha dhuluma katika uchaguzi,” Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka alisema.  

Raila alisema walisimamisha maandamano dhidi ya serikali ili kutoa nafasi kufanyika kwa mazungumzo lakini ikiwa utawala wa Rais William Ruto hautashirikiana, hawatasita kutangaza njia nyingine ya kuwasilisha malalamishi yao.

Maandamano ya hivi majuzi yalisababisha vifo vya watu kadhaa huku wengine wengi wakijeruhiwa. Kulingana na ripoti za mashirika ya kibinadamu wengi wa waliofariki walikuwa na majeraha ya risasi.

Idara ya polisi imelaumiwa kwa mauaji na kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

View Comments