In Summary
  • Waliokamatwa ni watu wawili ambao ni mmiliki wa nyumba ambapo gari la teksi la Muiruri lilipatikana ndani ya shamba la Kapsoya.
PATRICK MUIRURI DEREVA WA TEKSI ALIYEUAWA NA MWILI KUTUPWA KWENYE SHAMBA LA CHAI KERICHO

Dereva wa teksi mjini Eldoret ambaye alitekwa nyara na kutoweka siku mbili zilizopita amepatikana ameuawa.

Afisa mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Ainabkoi Alloys Mathoka alisema mwili wa Patrick Muiruri ulipatikana ukiwa umetupwa katika shamba la chai eneo la Chepsonoi  Kericho.

"Tunachunguza suala hilo ili kubaini jinsi marehemu alikumbana na kifo chake," alisema bosi huyo wa polisi.

Awali madereva wa teksi mjini Eldoret na familia ya marehemu waliandamana nje ya mahakama ya Eldoret baada ya washukiwa wawili waliokuwa wamekamatwa kuachiliwa kwa dhamana.

MCA wa Langas Peter Muya ambaye alikuwa na wahudumu wa teksi alisema inashangaza kuwa washukiwa hao waliachiliwa kabla ya dereva wa teksi kujulikana aliko.

Waliokamatwa ni watu wawili ambao ni mmiliki wa nyumba ambapo gari la teksi la Muiruri lilipatikana ndani ya shamba la Kapsoya.

Mke wa dereva wa teksi Grace Muiruri alisema mumewe alitoweka na juhudi zake za kumtafuta hazikufua dafu kwa sababu simu yake iliita bila kupokelewa.

Alisema hakuwa ameonyesha hofu yoyote kwa maisha yake.

Wenzake walisema Muiruri alikuwa amepigiwa simu na baadhi ya watu waliokuwa wakitaka huduma za teksi.

Aliondoka katika eneo lake la kuegesha magari huko Trakadero siku ya Ijumaa lakini hakurejea.

Polisi na wahudumu wa teksi walipongeza msako wa kulitafuta gari lake walifichua kuwa gari hilo liliendeshwa hadi kapsabet na kisha kurudi Eldoret.

Ilitafutwa hadi kwenye nyumba iliyoko Kapsoya Estate ambapo washukiwa walikamatwa.

Mathoka alisema washukiwa hao wawili ambao walikuwa wameachiliwa na mahakama watakamatwa tena kujibu mashtaka ya mauaji.

Mke wake alisema wana watoto wanne na walikuwa na matumaini kwamba mlezi wao atapatikana akiwa hai.

"Alikuwa mume mwenye upendo aliyejitolea kwa kazi yake na hakuwahi kumuudhi mtu yeyote," alisema Grace ambaye alizungumza baada ya washukiwa hao kuachiliwa na mahakama.

 

 

 

 

View Comments