Seneta wa Narok Ledama Olekina sasa anasema Seneti inafaa kutoa mafunzo ya miezi sita kwa Bunge la Kaunti ya Meru.
Katika sasisho kupitia Twitter mnamo Jumatatu, Novemba 6, Ledama alidokeza kuwa kungekuwa na mizozo ya mara kwa mara ikiwa mafunzo hayo hayatatolewa.
"Seneti inafaa kutoa mafunzo ya miezi sita kwa Bunge la Kaunti ya Meru la sivyo hii itakuwa tambiko la miezi sita," alisema Ledama.
Haya yanajiri siku chache baada ya wawakilishi Wadi wa Bunge la Kaunti ya Meru kumtimua kwa kauli moja Gavana Kawira Mwangaza kwa mara ya pili katika muda wa chini ya mwaka mmoja tangu kuchaguliwa.
Gavana Mwangaza anashutumiwa kwa utovu wa nidhamu, utumizi mbaya wa pesa za umma na kudharau bunge la kaunti.
Wanamshutumu Gavana Kawira kwa kupendelea jamaa wa familia katika nyadhifa kuu za kaunti, kufanya uteuzi kinyume cha sheria na maagizo ya mahakama, kwa kutozingatia taratibu zinazofaa za kuajiri, ikiwa ni pamoja na kutaja barabara ya umma kwa jina la mumewe bila kufuata taratibu za kisheria.
Kawira alitimuliwa na bunge la Kaunti kwa mara ya kwanza mnamo Desemba 2022.
Alinusurika baada ya Kamati Maalumu ya Seneti yenye wajumbe 11 iliyoteuliwa kuchunguza sababu za kushtakiwa kwake kueleza kuwa mashtaka ambayo yalikuwa yametolewa dhidi yake hayakuthibitishwa.
Hatima ya gavana huyo huru sasa iko kwa Seneti ambayo itampindua au kuunga mkono kuondolewa kwake.
Hoja ya kuondolewa mashtaka itasikizwa katika kikao cha Seneti baada ya mrengo wa walio wengi kupinga jaribio la upande wa walio wachache kutaka kesi hiyo kusikilizwa na kamati maalum ya wanachama 11.