In Summary

•Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya David Njeng'ere mnamo Alhamisi alitangaza kwamba usahihishaji bado unaendelea 

•Jumla ya watahiniwa 1,282,574 walisajiliwa na kufanya mitihani ya  KPSEA mwaka huu.

WAZIRI WA ELIMU EZEKIEL MACHOGU
Image: HISANI

Wanafunzi waliofanya mitihani yao ya Tathmini ya Elimu ya Shule ya Msingi ya Kenya (KPSEA) watalazimika kusubiri kwa muda majibu ya mitihani hiyo.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya David Njeng'ere mnamo Alhamisi alitangaza kwamba usahihishaji bado unaendelea kwani walilazimika kutanguliza mitihani ya  KCPE.

"Kwa wazazi na walezi ambao watoto wao walikalia mitihani ya  KPSEA, fahamu tu kwamba tulipaswa kutanguliza matokeo ya KCPE ili  kuafikia taratibu za jinsi wanafunzi hao watakapojiunga na kidato cha kwanza  kabla ya sherehe za Krisimasi," alisema.

Jumla ya watahiniwa 1,282,574 walisajiliwa na kufanya mtihani wa  KPSEA mwaka huu.

Njeng'ere aliangazia kuwa uwekaji alama unaendelea na matokeo yatatolewa kabla ya kuendelea na Shule ya Sekondari ya msingi(Junior school).

Alibainisha kuwa matokeo yatatolewa katika ripoti tatu; ya kila mwanafunzi, ripoti mahususi za shule na ripoti ya kitaifa ya tathmini ya msingi shuleni na muhtasari wa mitihani hiyo.

Ripoti ya kitaifa itaangazia maeneo yanayohitaji usaidizi pamoja na idadi ya wanafunzi katika kila kiwango cha ufaulu kwa kila mada inayohitaji usaidizi.

Ripoti ya shule ya kibinafsi itaundwa kulingana na kila shule na itaangazia maeneo ambayo wanafunzi wanakabiliwa na matatizo na ambapo shule zinahitaji usaidizi zaidi.

View Comments