In Summary

• Takriban wafanyakazi 32 wa mashamba kutoka Thailand waliuawa na wengine kadhaa kuchukuliwa mateka wakati Hamas ilipoishambulia Israeli mnamo tarehe 7 Oktoba.

• Tangazo hilo limezua hisia tofauti nchini Kenya, huku baadhi wakihofia usalama wa wafanyakazi hao.

• Israel ilisema kuwa wafanyakazi wa kigeni wana haki za ajira sawa na raia wa Israel.

Maelfu ya wafanyakazi wa shamba kutoka Thailand wameondoka Israeli tangu vita kuanza
Image: BBC

Kenya inawapeleka wafanyakazi 1,500 wa mashambani nchini Israel, wizara ya kazi imesema.

Tangazo hilo linakuja takriban wiki mbili baada ya Malawi kuwapeleka vijana 221 kufanya kazi katika mashamba ya Israel, na kusababisha lawama dhidi ya serikali.

Wafanyakazi hao wa kawaida watatumwa kwa kandarasi za miaka mitatu inayoweza kuongezwa, "na mapato ya uhakika" ya $1,500 (£1,195), wizara ya kazi iliongeza.

Israel imeigeukia Afrika ili kuziba pengo kubwa la wafanyakazi kwenye mashamba yake, baada ya kuondoka kwa wingi kwa wafanyakazi wa kigeni.

Zaidi ya wafanyakazi 10,000 wa mashambani wahamiaji - wengi wao wakiwa raia wa Thailand - wameondoka Israel tangu kuanza kwa vita na Hamas mapema mwezi Oktoba.

Israel pia imewazuia kufanya kazi wafanyakazi wa Kipalestina, ambao walikuwa karibu 20% ya nguvu kazi ya kilimo kabla ya vita.

Wizara ya kilimo ya Israeli iliiambia CNN wiki iliyopita kwamba inahitaji wafanyakazi wa mashamba kati ya 30,000 hadi 40,000.

Tangazo hilo limezua hisia tofauti nchini Kenya, huku baadhi wakihofia usalama wa wafanyakazi hao.

Takriban wafanyakazi 32 wa mashamba kutoka Thailand waliuawa na wengine kadhaa kuchukuliwa mateka wakati Hamas ilipoishambulia Israeli mnamo tarehe 7 Oktoba.

Wakosoaji pia wametilia shaka hali ambazo wafanyakazi watakabiliana nazo Israeli.

Makundi ya kutetea haki za binadamu kama Human Rights Watch awali yalielezea wasiwasi kuhusu jinsi Israel inavyowatendea wafanyakazi wa kigeni wa mashambani.

Israel ilikanusha inasema kuwa wafanyakazi wa kigeni wana haki za ajira sawa na raia wa Israel.

Baadhi ya Wakenya wameunga mkono mpango huo wakisema unatoa kazi zinazohitajika sana wakati ambapo Kenya inakabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira na kupanda kwa gharama ya maisha.

Kenya ina kiwango cha ukosefu wa ajira cha 5.5%, kulingana na Benki ya Dunia.

View Comments