In Summary

•Kampuni ya Safaricom inayongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Peter Ndegwa ilithibitisha kuwa huduma zote za M-PESA zimerejeshwa.

•Kampuni hiyo ilieleza kuwa matatizo ya kiufundi yanayoathiri huduma ya pesa kwa simu ya mkononi yalikuwa yameibuka.

CEO PETER NDEGWA
Image: MAKTABA

Kampuni kubwa zaidi ya kutoa huduma za simu za mkononi nchini Kenya, Safaricom PLC imevunja kimya baada ya huduma za M-pesa kurejeshwa.

Huduma za utumaji, utoaji na ulipaji pesa kupitia M-PESA zilikuwa zimetatizwa kwa zaidi ya saa moja siku ya Jumanne mchana na hivyo kuzua malalamiko mengi kutoka kwa Wakenya.

Katika taarifa iliyotolewa mwendo wa saa tisa na robo alasiri, kampuni hiyo inayongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Peter Ndegwa ilithibitisha kuwa huduma zote za M-PESA zimerejeshwa.

“Huduma zote za M-PESA sasa zinapatikana. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza na asanteni kwa uvumilivu wenu tulipofanya kazi ya kurejesha huduma," Safaricom ilisema katika taarifa.

Huduma za M-PESA zilirejeshwa Jumanne alasiri kufuatia malalamiko ya watumizi wengi wa simu ambao walishindwa kuzitumia.

Idadi kubwa ya watumiaji wa simu walikumbana na matatizo walipokuwa wakijaribu kutumia huduma za kutuma na kupokea pesa za M-pesa siku ya Jumanne asubuhi kwa kuwa miamala ilikuwa ikikosa kukamilika.

Wateja walipokea ujumbe wa arifa, “MPESA ina ucheleweshaji, na haiwezi kukubali ombi lako. Tafadhali subiri kwa dakika 10 kabla ya kujaribu tena,” kila walipojaribu kufanya miamala.

Watumiaji wengi wa MPESA walitumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kuwasilisha malalamishi yao kwa kampuni ya Safaricom  kuhusu huduma ya kutuma na kupokea pesa na kutafuta majibu kwa tatizo hilo.

"MPESA iko chini @safaricom_care @SafaricomPLC," mtumiaji wa Twitter @saagyn aliandika.

Katika jibu lake, Safaricom ilikiri kuwa huduma ya pesa kwa njia ya simu ilikuwa imekwama na kueleza kuwa tatizo hilo lilikuwa likitatuliwa.

“Hujambo. Tunasikitika kuwa kuna hitilafu kwa ujumla inayoathiri huduma za M-PESA kwenye STK na APP. Hili linashughulikiwa kwa kipaumbele cha hali ya juu. Samahani kwa usumbufu uliojitokeza,” kampuni hiyo ilijibu.

Kampuni hiyo ilieleza kuwa matatizo ya kiufundi yanayoathiri huduma ya pesa kwa simu ya mkononi yalikuwa yameibuka.

View Comments