In Summary

• Familia ya mwanamke huyo (ambaye utambulisho wake haujawekwa wazi) walitembelea chumba cha kuhifadhia maiti cha City, Nairobi siku ya Jumatatu na kumtambua.

Picha za uchunguzi zilinasa mshukiwa nje ya jumba huko Roysambu Jumamosi Januari 13, 2024.

Maafisa wa upelelezi wanasaka aliko mwanamume aliyehusika na mauaji ya kinyama ya mwanamke mwenye umri wa miaka 24 ambaye mwili wake uliokatwakatwa ulipatikana ukiwa umeingizwa kwenye mfuko wa plastiki eneo la Thika Road mjini Nairobi.

Pia imebainika mwanamume huyo alitumia msumeno kuukata mwili wa mwanamke huyo ambaye kichwa chake bado hakijapatikana.

Polisi wanashuku kuwa mwanamume huyo alikuwa amekodishwa na huenda alibeba kichwa cha marehemu kuthibitishia waliyomtuma kwamba alikuwa amekamilisha kazi.

Kwa kutumia picha za CCTV, na simu, polisi wamemweka mshukiwa katika eneo la Ruaka, Kaunti ya Kiambu ambako anaonekana kukaa kwa siku nyingi.

Wapelelezi walitembelea eneo hilo Jumatatu na kuomba picha za CCTV kwenye majengo kadhaa kama sehemu ya uchunguzi.

Hii itawawezesha kutambua mshukiwa ambaye picha yake ilinaswa nje ya ghorofa alimomuua mwanamke huyo.

Familia ya mwanamke huyo (ambaye utambulisho wake haujawekwa wazi) walitembelea chumba cha kuhifadhia maiti cha City, Nairobi siku ya Jumatatu na kumtambua.

Hata hivyo, kwa sababu sehemu muhimu za mwili hazikuwepo, walitakiwa kusubiri uchunguzi zaidi wa sampuli zilizokusanywa kutoka kwa mwili huo na ndugu wa karibu kabla hawajatoa taarifa yoyote juu yake.

Sababu ya tukio hilo bado haijajulikana, polisi walisema na kuongeza mshukiwa aliukata mwili wa mwanamke huyo na kuondoa viungo, mikono na kichwa kutoka kwenye kiwiliwili.

Kisha akafunga sehemu za mwili katika shuka na mfuko wa plastiki.

Kulikuwa na alama za msumeno kwenye mwili wakati polisi walipofika kuuchukua katika chumba cha kuhifadhia maiti. Pia ilibainika kuwa mwanamume huyo alikuwa amepiga simu ili kupanga chumba hicho kwa kutumia nambari ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mwanamke. 

Polisi wanasema mshukiwa huyo alipiga simu Jumamosi, Januari 13, saa tatu usiku kukodi chumba. Baada ya kukitazama kile chumba, alirudi dakika tano baadaye.Alirudi kwa wakala huyo ambaye alimtaka alipe Sh2,000 za usiku huo kupitia malipo ya simu ya mkononi lakini akasema akaunti yake ya simu ilikuwa na matatizo na angelipa tu pesa taslimu.  

Alimpigia simu mwenye nyumba tena na kumpa mhudumu simu aongee naye ili aruhusiwe kulipia chumba hicho kwa pesa taslimu, jambo ambalo limeonekana kuwa mbinu nyingine aliyotumia kuficha utambulisho wake, polisi walisema. 

Mwanamke aliwasili saa mbili usiku na kuwaambia walinzi kuwa anaungana na mshukiwa katika Jumba la Green House Apartment chumba B1. Kulingana na polisi na wasimamizi katika ghorofa hiyo, alitarajiwa kurudisha funguo Jumapili asubuhi lakini hakufanya hivyo.

View Comments