In Summary
  • Wahandisi na wafanyikazi wamekita kambi katika eneo hilo kukamilisha nyumba hiyo mpya kabla ya Alhamisi wakati mwili huo utaondolewa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Eldoret.
Image: KWA HISANI

Nyumba mpya inayojengwa kwa mshikilizi wa rekodi ya Dunia ya Marathon Kelvin Kiptum inakaribia kukamilika kabla ya kuzikwa kwake siku ya Ijumaa.

Rais William Ruto aliagiza kujengwa kwa nyumba hiyo katika shamba la Kiptum lililoko Naiberi kaunti ya Uasin Gishu.

Wahandisi na wafanyikazi wamekita kambi katika eneo hilo kukamilisha nyumba hiyo mpya kabla ya Alhamisi wakati mwili huo utaondolewa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Eldoret.

"Tuko kwenye ratiba na tutakamilisha nyumba kufikia Alhamisi," mmoja wa wahandisi katika eneo hilo alisema.

Wakati uo huo, timu ya maafisa wa mauaji kutoka makao makuu ya DCI wamefika Eldoret ili kuongeza uchunguzi kuhusu ajali iliyosababisha kifo cha mshikilizi wa rekodi ya mbio za dunia za Marathon.

Timu hiyo inazuru maeneo yote ambapo Kiptum alionekana mara ya mwisho kabla ya ajali hiyo iliyogharimu maisha yake na ya kocha wake.

Kamanda wa polisi kaunti ya Elgeyo Marakwet Peter Mulinge alisema uchunguzi unaendelea vyema.

"Tunaendelea na uchunguzi inavyotakiwa," Mulinge alisema.

Vyanzo katika timu ya uchunguzi vilisema wanaunda upya harakati za mwisho za Kiptum kabla ya ajali.

Maafisa hao wa mauaji pia walitarajiwa kuzuru eneo la ajali karibu na Flax kwenye barabara ya Eldoret-Ravine.

Pia watakagua gari la ajali ambalo lilivutwa hadi kituo cha polisi cha Kaptagat.

 

 

 

 

 

 

View Comments