In Summary

•Watu wasiojulikana walivamia chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Nakuru War Memorial na kuiba mwili wa mwanamke.

•Familia, ikiuliza kuhusu kulipa bili ya Sh921,000, ilimwendea msimamizi wa Hospitali ya War Memorial.

Chumba cha kuhifadhi maiti
Image: BBC

Polisi wanachunguza madai kwamba watu wasiojulikana walivamia chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Nakuru War Memorial na kuiba mwili wa mwanamke.

Mwili huo ulikuwa umehifadhiwa hapo kwa karibu miezi sita.

Polisi waliripoti kuwa malalamishi yaliwasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Kaptembwa katika eneo la Nakuru Magharibi kuhusiana na madai hayo.

Tukio hili ni la hivi punde zaidi katika mfululizo wa mizozo kuhusu umiliki wa kituo hicho.

Matroni wa hospitali hiyo, Patricia Musale, alieleza kuwa mwili huo wa mwanamke ulihifadhiwa katika kituo hicho tangu Septemba 2023 kutokana na kutoelewana kwa familia kati ya baba na watoto wake.

Mnamo Februari 15, 2024, mahakama iliwapa watoto ruhusa ya kumzika mama yao.

Familia, ikiuliza kuhusu kulipa bili ya Sh921,000, ilimwendea msimamizi wa Hospitali ya War Memorial.

Hata hivyo, mnamo Februari 20, watu wasiojulikana walivamia chumba cha kuhifadhia maiti na kuchukua mwili wa mwanamke huyo na kuuhamishia katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Nakuru.

Familia hiyo baadaye ingeuhamisha hadi Umash Funeral Home mnamo Februari 21, 2024.

Matroni wa hospitali hiyo alisema aliripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Kaptembo katika eneo la Nakuru Magharibi ambapo maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi.

Musale alisema mwili huo ulihamishwa bila nyaraka sahihi na bili isiyoeleweka.

Hospitali hiyo imekumbwa na mzozo kuhusu umiliki wa ardhi.

Serikali ya kaunti hiyo inadai kuwa sasa inamiliki hospitali hiyo hatua ambayo imelemaza shughuli zake huko.

View Comments