In Summary
  • Huldah Mahikizo, ambaye ni mhudumu wa afya katika hospitali ya Port Reitz iliyoko Kaunti ya Mombasa, alifariki alipokuwa ameingia kwenye nyumba yao iliyoshika moto ili kumwokoa mwanawe.
Image: KWA HISANI

Mwanamke katika eneo la Madzindani, Kaunti ya Kilifi na mwanawe mwenye umri wa miaka miwili walifariki katika mkasa wa moto uliotokea Jumatano jioni.

Huldah Mahikizo, ambaye ni mhudumu wa afya katika hospitali ya Port Reitz iliyoko Kaunti ya Mombasa, alifariki alipokuwa ameingia kwenye nyumba yao iliyoshika moto ili kumwokoa mwanawe.

Mapema wiki hii, Bi Mahikizo alikuwa miongoni mwa wahudumu wa afya walioshiriki maandamano ya mgomo wa madaktari jijini Nairobi.

Kulingana na wakazi walioshuhudia kisa hicho alikuwa katika duka lake la dawa wakati moto ulipozuka.

Moto huo uliteketeza chumba chake cha kulala ambako mtoto huyo alikuwa amelala, pamoja na mali ya thamani isiyojulikana iliyokuwa ndani ya chumba hicho.

Mumewe, Bw George Sewaali, alikuwa nyumbani kwa jirani mmoja wakati ambapo tukio lilitokea na alipofika kwenye tukio hakukuwa na lolote la kufanya.

“Wajenzi waliokuwa wakifanya kazi karibu pamoja na wanakijiji ndio walitusaidia. Mwanagu alikuwa amelala kama kawaida. Niliporudi nyumbani nilijaribu kumuita mke wangu ila hakukuwa na jibu lolote. Maafisa wa kukabiliana na moto walipokuja ndio tuliweza kuwafikia ila tulikuwa tumechelewa. Wote walikuwa wameshaaga dunia."

Kwa mujibu wa familia, kuna uwezekano kuwa Bi Mahikizo aliishiwa na hewa na kuanguka, kwani mwili wake ulipatikana katika bafu ya ndani ya chumba chao.

Katika juhudi za kutafuta mlango wa kuondoka chumbani, aliingia kwenye mlango wa choo, ambako alikutana na mauti.

Miili ya wawili hao ilikuwa imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Kilifi zikisubiri upasuaji.

Licha ya wakazi kueleza kuwa moto huo huenda ulisababishwa na hitilafu za nyaya za umeme, polisi wameeleza kuwa walikuwa wakifanya uchunguzi kubaini kiini cha moto huo.

 

 

View Comments