In Summary

•Sifuna alibainisha kuwa SRC imependekeza kuongeza Sh14k kwenye mshahara wake, jambo ambalo anadai hakuwahi kuomba.

•"Sitapigania 14k za ziada wakati nchi nzima inasema tunahitaji kupunguza mzigo wa walipa kodi, sitaki ikae hii ya 14k,' Sifuna alisema.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna
Image: HISANI

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amejiunga na Wakenya wengine kukashifu pendekezo la serikali la kuongeza mishahara kwa nyadhifa mbalimbali za kisiasa.

Hii ni baada ya ripoti kuibuka kuwa Tume ya Kurekebisha Mishahara (SRC) imependekeza nyongeza ya mishahara kwa Mawaziri, Wabunge, Maseneta, Magavana na MCAS.

Katika taarifa kwenye akaunti yake ya Twitter, Sifuna alibainisha kuwa SRC imependekeza kuongeza Sh14,000 kwenye mshahara wake wa useneta, jambo ambalo anadai hakuwahi kuomba.

“Tuweke wazi tunazungumza kuhusu nini hapa. SRC inapendekeza kuniongezea 14k kwenye mshahara wangu. Sikuomba. Sihitaji,” Sifuna alisema Jumatano asubuhi.

Akielezea sababu yake ya kukataa nyongeza ya mshahara, alisema, "Bado ni pesa, katika nchi ambayo watu wengi hawana mapato, lakini kwa mtazamo mimi hulipa karibu 300k katika kodi ya mapato kila mwezi."

Aliongeza, "Sitapigania 14k za ziada wakati nchi nzima inasema tunahitaji kupunguza mzigo wa walipa kodi, sitaki ikae hii ya 14k."

Imeripotiwa kuwa SRC imependekeza Mawaziri, Maseneta, Wabunge, MCAs na magavana  kupata nyongeza ya mishahara ya maelfu ya pesa.

SRC ilibainisha kwamba viwango vya mishahara ya maafisa hao vitaongezwa kuanzia Julai mosi, ambayo ni siku tatu zilizopita, kumaanisha tayari viwango hivyo vpya vimeshatekelezwa katika mishahara ua mwezi huu wa Julai.

Hapo awali, mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino alikosoa vikali hatua hiyo ya nyongeza ya mishahara kwa wanasiasa na maafisa hao wa serikali.

Licha ya kuwa mmoja wa wabunge watakaonufaika na nyongeza hiyo, Owino amekosoa vikali hatua hiyo akisema kwamba imekuja wakati mbaya ambapo Wakenya wengi wanahangaika kimaisha.

“Wabunge na maafisa wengine wa serikali hawafai kuongezwa hata sarafu moja. Inasikitisha kuongeza mshahara ilhali Wakenya hawana kazi, Wakenya hawana mitaji ya kuanzisha biashara, Wakenya hawana pesa za kulipia karo za shule, Hakuna pesa za dawa. Sema HAPANA kwa nyongeza ya mshahara,” Babu Owino alisema kupitia kurasa zake mitandaoni.

Kwa mujibu wa SRC, Wabunge na maseneta, ambao mshahara wa sasa ni Sh725,502, malipo yao yataongezwa hadi Sh739,600 kila mwezi.

Malipo ya magavana yamerekebishwa kutoka Sh957,000 hadi Sh990,000 huku yale ya Mbunge wa Kaunti (MCA) yakiongezeka kutoka Sh154,481 hadi Sh164,588 kila mwezi.

View Comments