In Summary

•Hakimu Gilbert Shikwe aliamuru kwamba ombi la polisi la kuwazuilia washtakiwa kwa siku 21 halikutoa sababu za msingi.

•Upelelezi tayari unaendelea ili kubaini nia ya kubeba vitu mbalimbali ambavyo Mwangi na wenzake walikamatwa navyo.

Mwanaharakati Boniface Mwangi na wengine wanne katika Mahakama ya Milimani, Julai 26, 2024
Image: DOUGLAS OKIDDY

Mwanaharakati Boniface Mwangi na wengine wanne wanaokabiliwa na mashtaka ya kuchapisha habari za uongo wameachiliwa kwa dhamana ya Sh20,000 pesa taslimu huku polisi wakiendelea kuwachunguza.

Hakimu mkuu wa Milimani, Gilbert Shikwe aliamuru kwamba ombi la polisi la kuwazuilia washtakiwa kwa siku 21 halikutoa sababu za msingi.

Washukiwa hao ni pamoja na Mwangi, Albert Wambugu, Robert Otieno, Pablo Chacha na Erot Franco.

"Kwa kuzingatia maelezo ya upande wa mashtaka na upande wa utetezi, naona kwamba hakuna sababu za msingi za kuwanyima dhamana washtakiwa. Ninawapa dhamana ya pesa taslimu Sh20,000 kila mmoja," Hakimu alisema.

Kesi hiyo itatajwa Agosti 26.

Watano hao wanachunguzwa kwa madai ya uchapishaji wa uwongo, kushiriki katika mkusanyiko usio halali na kuleta fujo kwa namna ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Katika maombi mbalimbali yaliyowasilishwa kortini, wapelelezi wanatafuta amri ya kuwashikilia ili kukamilisha uchunguzi wa uhalifu uliotajwa hapo juu.

Kurugenzi iliiambia Mahakama kuwa upelelezi tayari unaendelea ili kubaini nia ya kubeba vitu mbalimbali ambavyo Mwangi na wenzake walikamatwa navyo.

Zaidi ya hayo, uchunguzi unaendelea ili kubaini mahali ambapo jeneza jeupe na misalaba nyeupe vilitoka na mfadhili ni nani.

DCI ilisema kuwa makazi ya watano hao hayajulikani na kuwaachilia kunaweza kutatiza uchunguzi.

Washukiwa hao kupitia kwa mawakili wao wamepinga kuwekwa kizuizini.

Wanasema kuwa polisi wamewafikisha washukiwa hao mahakamani bila kufunguliwa mashtaka kwa hivyo ombi hilo halina msingi wowote.

Mahakama aliombwa kuwaachilia washukiwa wote kwa dhamana huku upelelezi ukiendelea.

View Comments