In Summary

•Kuria alifunua mipango yake siku ya Jumatatu baada ya kukutana na waziri mkuu wa zamani katika ofisi yake ya Capitol Hill jijini Nairobi.

•“Nilikutana na waziri mkuu wa zamani kwa mazungumzo kuhusu Mazungumzo ya Kitaifa na uamuzi wa Chama Cha Kazi kujiunga na Muungano wa Azimio,” Kuria alisema .

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga
Image: HISANI

Moses Kuria, waziri wa zamani wa Huduma ya Umma, ametangaza nia yake ya kujiunga na Muungano wa Azimio wa Raila Odinga.

Kuria alifunua mipango yake siku ya Jumatatu baada ya kukutana na waziri mkuu wa zamani katika ofisi yake ya Capitol Hill jijini Nairobi.

Tangazo hili linajiri kufuatia kuondolewa kwa Kuria kutoka kwenye Baraza la Mawaziri la Rais William Ruto wakati wa uundaji mpya wa baraza hilo.

“Nilikutana na waziri mkuu wa zamani kwa mazungumzo kuhusu Mazungumzo ya Kitaifa na uamuzi wa Chama Cha Kazi kujiunga na Muungano wa Azimio,” Kuria alinukuliwa na kituo kimja cha redio humu nchini kupitia mazungumzo ya simu.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wake wa kujiunga na Azimio, Kuria alieleza kuwa ni ishara ya imani yake katika serikali yenye uwakilishi mpana ya Rais Ruto, ambayo sasa inashirikiana kwa karibu na Odinga.

“Kukutana kwangu na Odinga ni uthibitisho wa imani yangu katika serikali yenye uwakilishi mpana iliyo sasa na umoja wa nchi,” aliongeza katika mahojiano kwa simu baada ya mkutano.

Kuria alikuwa miongoni mwa mawaziri walioondolewa katika mabadiliko ya hivi karibuni yaliyosababishwa na maandamano ya GenZ.

“Tulichunguza masuala mbalimbali yanayokabili taifa. Nilimshukuru '''Baba'' kwa mara nyingine tena kwa kuchukua hatua ya kurejesha nchi mbali na anguko,” Kuria alisema.

Katika kuunda serikali yenye uwakilishi mpana, Rais Ruto alimteua wanachama wanne wa juu wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) katika Baraza lake la Mawaziri.

Wateule hao ni mwenyekiti wa chama John Mbadi (Hazina), Wycliffe Oparanya (Mikopo), Hassan Joho (Madini), na Beatrice Askul Moe (Jumuiya ya Afrika Mashariki).

Kuria alieleza kuunga mkono kwa dhati uamuzi wa Rais Ruto na Odinga wa kushirikiana, na kuunga mkono mazungumzo ya kitaifa ya kushughulikia changamoto zinazojirudiarudia nchini.

“Tulikubaliana kuwa hatuwezi kuendelea kutumia Panadol wakati tunahitaji upasuaji.

Mazungumzo ya kitaifa yajayo lazima na yatakuwa na marekebisho makubwa ya kimuundo kwa suluhisho la kudumu.

Tutafanya kazi kwa karibu katika jitihada hii huku tukishauriana na viongozi wengine wenye mtazamo sawa,” alisema Kuria baada ya mkutano na Odinga.

View Comments