In Summary

•Kuna hali ya wasiwasi inayoongezeka miongoni mwa wazazi ambao watoto wao bado hawajajulikana walipo.

Image: BBC

Mamlaka nchini Kenya zinasema uchunguzi wa vinasaba (DNA) utaanza Jumatatu ili kubaini miili ya watoto 18 waliofariki katika mkasa wa moto katikati mwa Kenya.

Kuna hali ya wasiwasi inayoongezeka miongoni mwa wazazi ambao watoto wao bado hawajajulikana walipo.

Naibu Rais Rigathi Gachagua alitangaza jana kuwa watoto 70 bado hawajatambuliwa kufuatia tukio hilo katika shule ya msingi ya Hillside Endarasha katika Kaunti ya Nyeri.

Hata hivyo, msemaji wa serikali Isaac Mwaura alitoa takwimu tofauti katika mkutano na wanahabari siku ya Jumamosi.

"Idadi tunayoweza kuthibitisha ni kwamba tuna vifo 18. Tulikuwa na watoto 156 katika bweni hilo. Takwimu nyingine sio za kutosha. Huwezi kusema 20, 30 au 40 hata 70 kwa sababu hiyo itakuwa ya kupotosha," alisema.

Ndugu ambao wamekuwa wakipiga kambi katika shule hiyo wakisubiri habari kuhusu watoto wao walitaka majibu kutoka kwa mamlaka.Maafisa wa serikali wametoa wito kwa wale waliosaidia kuwaokoa wanafunzi kuwarudisha watoto shuleni ili kusaidia katika kufuatiliaji. Shirika la Msalaba Mwekundu limeanzisha dawati la kufuatilia na pia linatoa msaada wa kisaikolojia kwa wale walioathirika.Watoto wanne bado wanaendelea kupata matibabu katika hospitali mbalimbali, huku hali yao ikiripotiwa kuwa shwari.

Moto huo wa shule umezua mjadala mkubwa kuhusu hatua za usalama katika shule mbalimbali nchini, ikizingatiwa kuwa shule kadhaa ziliwahi kukumbwa na mkasa wa moto.

Waziri wa Elimu Julius Migosi Ogamba alisema serikali itafanya itatathimini miongozo ya usalama na kuhakikisha utekelezaji wake unafuatwa.

View Comments