In Summary

•Makubaliano yaliafikiwa kufuatia mkutano kati ya Waziri Davis Chirchir, Viongozi wa Muungano wa wafanyakazi na katibu wa Cotu Francis Atwoli.

Abiria wakiwa wamekwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) huku wafanyakazi wakigoma mnamo Septemba 11, 2024.
Image: FELIX KIPKEMOI

Wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini Kenya watarudi kazini baada ya kuafikia makubaliano na serikali.

Iliripotiwa kwamba makubaliano yaliafikiwa kufuatia mkutano kati ya Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir, Viongozi wa Muungano wa wafanyakazi na katibu wa Muungano wa wafanyakazi nchini Kenya Cotu Francis Atwoli.

Hii ina maana kwamba operesheni za kawaida sasa zitarudi katika viwanja vya ndege vya JKIA pamoja na vile vya Mombasa, Kisumu na Eldoret baada ya huduma kulemazwa huku baadhi ya mashirika ya ndege yakipata hasara kubwa.

Foleni ndefu zilishuhudiwa huku mamia ya wasafiri waliokwama wakisubiri, na kuathiri shughuli za ndege katika uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi zaidi Afrika Mashariki.

Picha kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha idadi kubwa ya abiria wakijaribu kuchukua mizigo yao katika uwanja wa JKIA huku mgomo huo ukianza kuamkia Jumatano.

Katika makubaliano hayo ya kurudi kazini kwa wafanyakazi hao, serikali itaruhusu uchunguzi wa stakhabadhi kuhusu ukodishaji wa miaka 30 wa uwanja wa ndege wa JKIA na kampuni ya India ya Adani.

Waziri wa Uchukuzi Chirchir ameahidi kwamba mkataba ulioafikiwa kati ya serikali na kampuni ya Adani utawasilishwa mahakamani ambapo serikali imeshtakiwa ili kuruhusu uchunguzi wa wazi.

Katika makubaliano hayo yaliosomwa na Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli, waliamua kuwapatia wafanyakazi hao wa viwanja vya ndege siku 10 kuchunguza stakhabadhi hizo za Adani kabla ya mkutano mwengine kufanywa na washikadau.

Vilevile Atwoli amesema kwamba serikali imekubali kuanzisha mazungumzo ya mishahara na wafanyakazi mbali na makubaliano mapya ya majadiliano katika kipindi cha miezi miwili.

View Comments