In Summary

•Kinyua alisema kuwa mkasa huo ulimshtua na kumuacha katika hali ya huzuni kwani hakuwahi kutarajia jambo kama hilo kutokea.

•"Mimi ni mzazi, na tumekaa na hawa watoto miaka mingi, tumekuwa nao miaka 13, na tumezoeana na wao," alisema.

Bw David Kinyua, mmiliki wa Hillside Endarasha Academy akizungumza mnamo Septemba 17, 2024.
Image: HISANI

Bw David Kinyua, mkurugenzi wa shule ya Hillside Endarasha Academy, amebainisha kuwa amehuzunishwa sana na mkasa wa moto wa hivi majuzi katika shule hiyo ambao uliangamiza wavulana ishirini na mmoja na kuwaacha wengine wachache wakiuguza majeraha.

Akiwahutubia na waandishi wa habari siku ya Jumanne, mfanyabiashara huyo alitangaza kuwa mkasa huo ulimshtua na kumuacha katika hali ya huzuni kwani hakuwahi kutarajia jambo kama hilo kutokea.

Kinyua alibainisha kuwa alikuwa ameishi na wanafunzi kwa zaidi ya muongo mmoja na walikuwa na uhusiano mzuri sana wa karibu.

“Nimeathirika sana na hii kitu kwa sababu si kitu nilikuwa natarajia. Mimi ni mzazi, na tumekaa na hawa watoto miaka mingi, tumekuwa nao miaka 13, na tumezoeana na wao,” Bw Kinyua alisema.

Mfanyibiashara huyo kutoka kaunti ya Nyeri sasa ametoa wito kwa watu kusimama nao katika wakati huu mgumu ili kuwasaidia wapone haraka.

“Hata mimi nimehuzunika sana, na pia ata mimi ndiye nimekufiwa na watoto wengi.Naomba Mungu tu, na kila mtu nawaomba mtushikilie na mtusaidie na maombi ili tupone haraka,” alisema.

Kuhusu hatua ambazo taasisi hiyo imechukua kuwasaidia wanafunzi hao kukabiliana na athari ya mkasa huo wa kusikitisha uliogharimu maisha ya wenzao, Bw Kinyua alisema kuwa bweni jipya linajengwa mbali na mahali ambapo bweni lililoteketea lilikuwa.

“Tumetoa bweni mahali ilikuwa, tunataka kuipeleka mahali kwingine. Tumebadilisha hadi njia mahali watoto watakuwa wanapitia, haswa wavulana ili hawatakuwa na shida na kiwewe kupitia mahali ile bweni ilikuwa,” alisema.

Kinyua alifichua kuwa wamepanga kikao kati ya shule, wazazi, viongozi wa kanisa kati ya wadau wengine mbalimbali kwa juhudi za kujadili njia ya kusonga mbele.

Pia alizungumza kuhusu mipango ya kupunguza idadi ya wanafunzi wanaolala katika shule hiyo ambapo alifichua kuwa wanafunzi wa bweni watapunguza kutoka wanafunzi 330 hadi 195.

“Tumepanga, kwa sababu hatuna ni pamoja na wanafunzi wa bweni, tumeona watoto wale wa karibu kwanza wawe wanarudi nyumbani ili tuweze kuwa na wachezaji wachache kwenye bweni,” Bw Kinyua siku ya Jumanne.

Alisema kwa sasa kuna bweni la wavulana 97 katika kituo hicho, na wasichana 98.

“Hao wengine watakuwa wanafunzi wa kutwa. Kitambo walikuwa wavulana 164 na wasichana 166,” alisema.

Hatua hiyo inajiri huku shule hiyo ikijaribu kurudisha shughuli za kawaida, baada ya kukumbwa na maafa yasiyosahaulika.

View Comments