In Summary

• Rais William Ruto amefanya mkutano na wabunge wa kaunti ya Nyeri na kuafikiana kubadilisha hospitali hiyo kuwa shirika la serikali.

• Hospitali ya Mwai Kibaki - Othaya imeorodheshwa kati ya haospitali muhimu za kutoa huduma za afya katika mpango wa huduma ya afya kwa wote UHC unaoanza mwezi Oktoba

Hospitali ya Mwai Kibaki
Image: Lemiso Sato Emmanuel

Rais William Ruto  amesema kuwa hospitali ya Mwai Kibaki ya Othaya itabadilishwa na kuwa shirika huru la serikali na kuacha kuwa chini ya usimamizi wa hospitali kuu ya Kenyatta.

Rais Ruto alisema kuwa utekelezwaji huo utachapishwa kwenye gazeti la serikali na bodi ya usimamizi kuteuliwa na kupewa bajeti yake huru.

Uamuzi huu umejiri baada ya mkutano kati ya Rais William Ruto na wabunge kutoka kaunti ya  Nyeri ambapo walikubaliana kuendeleza miradi mingine ya barabara, viwanja, masoko ya mazao na mipango ya maji.

Mkutano huo ulifanyika katika Ikulu ya Nairobi Jumatano tarehe 18.

Kulingana na Rais Ruto, kupandishwa kwa hadhi ya hospitali hiyo kutaimarisha utoaji huduma wa taasisi hiyo, kutokana na kuboreshwa kwa vifaa na wahudumu. 

Hospitali ya Mwai Kibaki - Othaya imeorodheshwa kati ya haospitali muhimu za kutoa huduma za afya katika mpango wa huduma ya afya kwa wote UHC unaoanza mwezi Oktoba.

Mpango wa UHC unalenga kuhakikisha kuwa Wakenya wanapata na kupokea huduma za hali ya juu za afya bila kisiki cha kifedha.

Mpango wa UHC unaanza sambamba na kubadilishwa kwa Hazina ya kitaifa ya afya (NHIF)  kuwa mamlaka ya afya ya umma (SHA).

SHA ilibuniniwa kwa madhumuni ya kutoa huduma za afya bora kwa kila mkenya.

View Comments