In Summary

•"Tumepokea matokeo ya DNA ya wahasiriwa 21 wa moto katika Chuo cha Hillside Endarasha, na miili yote 21 imetambuliwa kupitia DNA," Oduor alisema.

•Uchunguzi wa maiti ulifanywa na Oduor, akisaidiwa na wataalam wengine wa uchunguzi.

Hillside Endarasha Academy ambapo wanafunzi 17 walifariki katika kisa cha moto mnamo Septemba 17, 2024.
Image: Wangare Mwangi// KNA

Miili yote ya waathiriwa wa mkasa wa moto wa Hillside Endarasha Academy imetambuliwa vyema, mwanapatholojia wa Serikali Johansen Oduor amesema.

Mkasa huo wa moto uligharimu maisha ya wavulana 21 na kuwaacha takriban wengine 14 wakiuguza majeraha.

Akizungumza Jumatano, Oduor alisema wameanza shughuli ya kuwasiliana na familia za marehemu.

"Tumepokea matokeo ya DNA ya wahasiriwa 21 wa moto katika Chuo cha Hillside Endarasha, na miili yote 21 imetambuliwa kupitia DNA," alisema.

Oduor alisema timu inayojumuisha Kurugenzi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai, Shirika la Msalaba Mwekundu, na washauri wanasaidia familia katika mchakato wa mazishi.

"Mkemia wa serikali aliweza kulinganisha sampuli zilizopatikana kutoka kwa miili ya wahasiriwa na wazazi."

Uchunguzi wa maiti ulifanywa na Oduor, akisaidiwa na wataalam wengine wa uchunguzi.

Ukusanyaji wa sampuli za DNA kwa madhumuni ya kutambua waathiriwa ulianza Jumatatu wiki jana.

Chanzo cha moto katika shule hiyo bado hakijajulikana, lakini makachero wa DCI wanafanya kazi ya kutegua kitendawili hicho.

Wiki iliyopita, Msemaji wa Serikali Issac Mwaura alisema wanafunzi wote walioathiriwa na kisa hicho cha moto wamehesabiwa.

"Wasichana wote wako nyumbani na wazazi wao huku wavulana wote 164 wamehesabiwa," alisema.

Mwaura alitaja msiba wa kusikitisha wa wanafunzi 21 kama janga lisiloweza kuwaziwa.

"Wavulana wawili walikufa hospitalini walipokuwa wakipatiwa matibabu, na miili mingine 19 ilitolewa kutoka kwa bweni lililoungua," alisema.

Mnamo Jumanne, mmiliki na mkurugenzi wa Hillside Endarasha Academy, David Kinyua, alisema shule hiyo itapunguza idadi ya wanafunzi wa bweni.

Kinyua alisema hatua hiyo itasaidia kutengeneza nafasi shuleni ili kuchukua wanafunzi.

Kulingana na yeye, idadi ya mipaka itapunguza kutoka kwa wanafunzi 330 hadi 195.

View Comments