In Summary

•Easy Coach imeondoa marufuku iliyokuwa imeweka kwa usafirishaji wa samaki kama mizigo ya abiria kwenye mabasi yake.

•Kampuni hiyo hapo awali ilikuwa imepiga marufuku usafirishaji wa samaki kama mizigo ya abiria kwenye mabasi yake.

Image: EASY COACH FACEBOOK

Kampuni ya uchukuzi ya Easy Coach imeondoa marufuku iliyokuwa imeweka kwa usafirishaji wa samaki kama mizigo ya abiria kwenye mabasi yake.

Katika taarifa ya Jumanne jioni, kampuni hiyo iliweka wazi kuwa abiria sasa wanaruhusiwa kubeba aina mbalimbali za samaki kwenye mabasi yao mradi wanazingatia maagizo fulani yaliyotolewa.

Easy Coach iliwaomba abiria wanaosafiri na mizigo yao kubeba samaki kama mizigo ambayo imepakiwa ipasavyo.

"Kusimamishwa kumeondolewa na sasa unaweza kubeba samaki wako aliyekaanga, kavu, aliyepitishwa kwa moshi, ama kutiwa chumvi; aina ya mbuta, ngege, kamongo, omena n.k, TU kama mizigo iliyobenwa kwenye mabasi yetu kwa sharti ya kuwa imefungwa ipasavyo,” Easy Coach ilisema.

Kampuni hiyo hapo awali ilikuwa imepiga marufuku usafirishaji wa samaki kama mizigo ya abiria kwenye mabasi yake.

Marufuku hiyo ilifuatia malalamiko mengi yaliyotolewa na baadhi ya wateja kuhusu samaki na bidhaa za samaki ambazo hazijafungashwa vizuri ambazo zilidaiwa kuchafua mizigo yao.

Katika notisi ya awali iliyotolewa kwa wasimamizi wote wa matawi mnamo Agosti 11, Kampuni hiyo haikutoa maelezo kuhusu ni kwa nini iliweka marufuku hiyo ikisema tu hili limekuwa "kero" miongoni mwa wateja wake. 

"Tunapenda kukufahamisha kwamba kuanzia sasa samaki na bidhaa zake zote ni marufuku kwenye mifumo yote ya usafiri wa Easy Coach iwe ikiambatana na abiria au kwa vifurushi," notisi hiyo ilisema.

Kuingana na notisi hiyo, agizo hilo lilifaa kuanza kutekelezwa mara moja na watumiaji wote kutakiwa kuizingatia. 

"Inatarajiwa kwamba mtashirikiana na maagizo ya kuzuia matatizo yanayohusiana," ilisomeka.

Agizo hilo lilikaribishwa kwa hisia mseto huku baadhi ya Wakenya wakionekana kuikosoa kampuni hiyo ya uchukuzi kuhusu hatua hiyo. 

View Comments